Mapigano yazuka upya Darful, saba wauawa

Muktasari:
- Mapigano ya kikabila mara nyingi huzuka huko Darfur, eneo lenye ukubwa wa Ufaransa ambalo liliharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2003. Takriban watu 300,000 waliuawa na milioni 2.5 kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN).
Dar es Salaam. Mapigano makali kati ya makundi ya waarabu na wasio waarabu katika jimbo la Darfur nchini Sudan yamesababisha vifo vya watu saba.
Vyombo vya habari nchini Sudan leo Desemba 24, 2022 vimetangaza ghasia zilizozuka siku ya Jumatano Desemba 21 karibu kilomita 20 kutoka mji mkuu wa jimbo la Darfur, Nyala.
Ghasia hizo zilikua ni baina ya wafugaji wa kiarabu dhidi ya wakulima kutoka jamii ya wachache ya Daju na makabila mengine yasiyo ya waarabu.
Kituo kimoja cha habari nchini humo kimeeleza kwamba haijabainika mara moja ni nini kilichochea mapigano hayo.
“Kundi la wafugaji waliokuwa wakiendesha ngamia na magari walishambulia kijiji cha Amuri Ijumaa iliyopita na kuacha eneo hilo likiteketezwa na watu wanne kuuawa,” shirika la habari la SUNA lilisema.
Shirika la habari la AFP limeeleza baadhi ya watu wengine waliuawa wakati mapigano hayo yalipoenea hadi katika vijiji vya karibu ambavyo vilikuwa vimetelekezwa.
Takriban watu 20 walitibiwa katika hospitali ya Nyala kutokana na majeraha ya risasi, hata hivyo vikosi vya usalama vilitumwa katika eneo hilo kudhibiti ghasia.
Mapigano ya kikabila mara nyingi huzuka huko Darfur, eneo lenye ukubwa wa Ufaransa ambalo liliharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2003.
Mzozo huo ulikutanisha waasi wa makabila madogo madogo dhidi ya serikali iliyotawaliwa na waarabu pamoja na Rais wa wakati huo, Omar al-Bashir.
Takriban watu 300,000 waliuawa na milioni 2.5 kukimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN).
Wakati mzozo huo ukiwa umepungua, ghasia bado zinapamba moto kati ya wafugaji wa kuhamahama na wakulima wasio na makazi juu ya upatikanaji wa maji na uhaba na ardhi ya malisho.
Sudan bado inapambana na matokeo mabaya ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan Oktoba 2021.