Mfanyabiashara aoa wake saba kwa mpigo, wamo ndugu wawili

Muktasari:

  • La kushtua zaidi kwenye ndoa hiyo ni uwepo wa ndugu wawili wa damu wengine ni pamoja na Mariam, Madina, Aisha, Zainabu, Fatuma, Rashida, na Musanyusa ambaye ni mke wa kwanza wa tajiri huyo na amedumu naye kwa miaka saba.

Uganda. ‘Mwamba huyu hapa,’ ndivyo unavyoweza kusema, Ssaalongo Nsikonenne mfanyabiashara kutoka Uganda ameingia kwenye vichwa vya habari baada ya kuoa wake saba kwa mpigo.

La kushtua zaidi kwenye ndoa hiyo ni uwepo wa dada wawili ambao ni ndugu wa damu wengine ni pamoja na Mariam, Madina, Aisha, Zainabu, Fatuma, Rashida, na Musanyusa ambaye ni mke wa kwanza na amedumu naye kwa miaka saba.

Kwa mujibu wa tovuti ya igbere news walifunga ndoa na sherehe ya harusi ilifanyika katika Kijiji cha Bugereka wilayani Mukono Jumapili, Septemba 10, 2023.

Nsikonenne ambaye anatajwa kama mfanyabiashara tajiri nchini humo alifunga ndoa majira ya saa mbili asubuhi baada ya maharusi kwenda saluni huku wakiwa kwenye magari yenye namba zilizoandikwa majina yao kila mmoja.

Baada ya kula kiapo, Nsikonnene na wake zake saba waliondoka na msafara mkubwa wakipita katika miji ya Kalagi, Kasana, na Nakifuma, huku wakipambwa na  waendesha bodaboda wakielekea nyumbani.

Katika kuonyesha upendo kwa wake zake hao bwana huyo aliwanunulia magari mapya kila mmoja huku akiwasifu kwa uaminifu wao. Na kuahidi kuongeza wake zaidi siku zijazo.

"Mimi bado ni kijana na katika siku za usoni, Mungu akipenda, siwezi kusema huu ndio mwisho wake, nitaongeza wake wengine," aliongeza.

Kwa mujibu wa baba yake bwana harusi, Hajj Abdul Ssemakula, ndoa ya wake wengi imekuwa ni desturi katika familia yao, akiongeza kuwa babu yake alikuwa na wake sita alioishi nao katika nyumba moja.

"Marehemu baba yangu alikuwa na wake watano, na mimi mwenyewe nina wake wanne ambao wanaishi katika nyumba moja," amesema