Papa Francis alazwa, hofu yatanda kukosekana Jumapili ya Matawi

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis amelazwa hospitalini tangu jana Jumatano kutokana na tatizo ya kupumua lililomuanza hivi karibuni, na ataendelewa kupatiwa matibabu kwa siku kadhaa za matibabu.

Taarifa iliyotolewa leo Machi 30, 2023, Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni amesema kwamba Papa mwenye umri wa miaka 86 anasumbuliwa na tatizo la kupumua ambalo ni la kawaida na siyo Uviko 19.

Hii ni mara ya kwanza kwa Francis kulazwa hospitali tangu alipokaa siku 10 katika Hospitali ya Gemelli Julai mwaka wa 2021 na kufanyiwa upasuaji kwenye tumbo.

Maswali yameibuka kuhusu hali ya afya ya Francis na uwezo wake kusherekea matukio ya kanisa wiki hii na Jumapili ya matawi.

Chanzo kutoka Vatican kimethibitisha kwamba  shughuli za Papa kwa siku ya leo Alhamisi zimesitishwa, wakati huu ambao kumegubikwa shughuli nyingi kwa Papa kuelekea sikukuu ya Pasaka.

Licha ya uzee na changamoto za kiafya, Papa Francis ameendelea kusafiri, ambapo mapema mwaka huu alifanya ziara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini na kulakiwa na mamia kwa maelfu ya waumini, viongozi na wakuu wa nchi hizo.

Mwezi ujao, anatarajiwa kutembelea Hungary na kukutana na Waziri Mkuu, Viktor Orban.