Polisi adaiwa kujiua kwa kujipiga risasi mdomoni
Muktasari:
- Ofisa wa Polisi adaiwa kujiua kwa kujipiga risasi nyumbani kwake katika Kaunti ya Murang’a nchini Kenya, huku sababu ya kujiua ikiwa bado haijafahamika.
Dar es Salaam. Katika tukio la kushangaza, Polisi nchini Kenya wanachunguza kifo cha ofisa wake anayedaiwa kujipiga risasi mdomoni ambayo ilitokea nyuma ya kichwa chake.
Tukio hilo limetokea alasiri ya Jumatatu Novemba 20, katika makazi ya askari huyo ambayo yako karibu na Kituo cha Polisi Nyakianga, ambacho marehemu alikuwa anafanyia kazi katika Kaunti ya Murang’a.
Taarifa iliyoripotiwa na tovuti ya Tuko ya nchini humo, imesema ripoti ya polisi imeeleza kuwa ofisa mwenziye alisikia mlio wa risasi hali iliyomlazimu kwenda mahali ambako ulisikika ili kujua nini kimetokea.
"Alipofika alikuta marehemu amejipiga risasi kwa kutumia bunduki yake ya G3 huku mwili wake ukiwa umelala kwenye dimbwi la damu kitandani kwake," ripoti hiyo imeeleza.
Taarifa zaidi zimesema mwili huo umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Misheni ya Kiria-ini, ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.