Raila Odinga awekwa kizuizini-9

Mwaka 1982 Raila Odinga (kulia) alihukumiwa kifungo kwa kosa la kujadiliana na Hezekiah Ochuka kuipindua Serikali.

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi wanajeshi, wahadhiri wa vyuo na wanafunzi walivyokamatwa baada ya mapinduzi kushindwa, miongoni mwa waliokamatwa alikuwa Raila Odinga.

Jana tuliona jinsi wanajeshi, wahadhiri wa vyuo na wanafunzi walivyokamatwa baada ya mapinduzi kushindwa, miongoni mwa waliokamatwa alikuwa Raila Odinga.

Mapinduzi hayo yalishindikana kwa sababu askari wengi hawakutekeleza sehemu za mpango huo, wengine walikuwa wakinywa pombe na kupora badala ya kwenda kumkamata Rais na mawaziri wake.

Waasi hao hawakuwa wamejiandaa kukabiliana na mashambulizi yoyote baadaye waliposhambuliwa na vikosi vya wanajeshi wanaoitii Serikali.

Walishindwa kumkamata kiongozi yeyote wa siasa waliyekuwa wamemlenga na wala hawakuteka makao makuu ya jeshi na ya polisi kama walivyokuwa wameweka kwenye mipango yao.

Walishindwa kwa sababu askari wa Jeshi la Anga la Kenya (KAF) hawakuungwa mkono na wanajeshi wenzao wa vikosi vingine. Ndani ya siku mbili baada ya mapinduzi kushindwa, karibu askari wote 2,000 wa KAF walikuwa wamekamatwa. Kesi zilipopelekwa Mahakama ya Kijeshi, zaidi ya 1,000 walipatikana na hatia ya uchochezi, uhaini au uhalifu.

Walishtakiwa katika Mahakama ya Kijeshi katika Kambi ya Jeshi ya Lang’ata Nairobi. Askari wa kwanza kukutwa na hatia ya uhaini ni Koplo Bramwell Njereman aliyekuwa na miaka 27.

Mahakama ilisema Koplo Njereman alifikiria, alipanga, alibuni au alikusudia yeye na wengine kupindua Serikali ya Kenya kwa njia zisizo halali.

Koplo Njereman alidaiwa kuwa, ndiye aliandaa makombora ya kwenda kulipuliwa Ikulu ya Nairobi na aliyasimamia yakiingizwa kwenye ndege za kivita, akamlazimisha rubani kwa mtutu wa bunduki kuendesha mpango wa ulipuaji huo kwa kutumia ndege ya kijeshi aina ya F-5.

Koplo Njereman alishutumiwa kuhudhuria mkutano Julai 17, 1982 ambao Hezekiah Ochuka aliwaeleza namna ya kuwapata askari wengine kwa ajili ya kushiriki mapinduzi. Katika utetezi wake, Koplo Njereman alisema hakujiunga na njama za mapinduzi hayo kwa hiari bali alikuwa akitekeleza amri kutoka kwa wengine.

Mahakama ilisema miongoni mwa vitendo vilivyothibitika vya kumtia hatiani Koplo Njereman ni kumlazimisha Meja David Mutua kurusha ndege aina ya F-5 kwenye misheni ya kulipua maeneo ya kimkakati hadi Nairobi.

Mashahidi 17 walitoa ushahidi dhidi yake na alihukumiwa kunyongwa. Takriban mwezi mmoja baadaye, Desemba 16, 1982 Koplo Walter Odira Ojode akawa Mkenya wa pili kupatikana na hatia ya kosa kama la Koplo Njereman katika Mahakama hiyo hiyo.

Mahakama ilieleza kuwa, Koplo Ojode aliwafungia ndani wanajeshi na maofisa wa jeshi na kuwaamuru Meja David Mutua na Kapteni John Mugwanja kurusha ndege za F-5 ili kulipua baadhi ya maeneo Nairobi. Yeye pia alihukumiwa adhabu ya kifo.

Wakati hayo yakiendelea, Koplo Amos Kunikina Marani alishtakiwa kwa kuzifanyia matengenezo ndege aina ya F-5 na kusaini fomu 700 kuthibitisha ndege hizo ziko tayari kuruka.

Koplo Marani alikiri kosa la uasi na alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela. Mahakama nyingine ya kijeshi iliwahukumu wanajeshi vifungo mbalimbali na kufikisha idadi ya wanajeshi 656 waliopatikana na hatia ya uasi katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoshindwa.

Raila Odinga ambaye baadaye alikuwa Waziri Mkuu wa Kenya, akiwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka wa 1982, walishutumiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na waliopanga mapinduzi.

Odinga alishtakiwa kwa uhaini, shtaka ambalo baadaye lilitupiliwa mbali.

Odinga na mshtakiwa mwenzake, mwanahabari Otieno Mak’onyango na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Alfred Vincent Otieno ambaye nyumba yake ilikuwa kituo cha kuendeshea mipango ya mapinduzi, waliwekwa kizuizini kwa miaka sita.

Katika kitabu chake alichokiita ‘Raila Odinga: The Flame of Freedom’, Odinga ametaja mashtaka 11 aliyoshtakiwa nayo mahakamani.

Katika shtaka la kwanza, Julai 1982, akiwa Nairobi, Odinga alimpa Private Hezekiah Ochuka gari aina ya ‘Peugeot 504’, lenye namba za usajili KVZ 642, ili kumsaidia kufanya maandalizi ya kupindua Serikali ya Daniel Toroitich arap Moi.

Shtaka la pili la Julai 18, 1982, Odinga alitembelea nyumba ya Ochuka iliyoko Umoja Estate jijini Nairobi na kujadiliana kuhusu mipango ya kupindua Serikali akiwa na Sajenti wa KAF.

Pia, alishtumiwa kuwa, Julai 30 1982 alikwenda katika Baa ya Little Eden iliyoko Umoja Estate jijini Nairobi na kujadiliana na Ochuka na wanajeshi wengine kutoka KAF kuhusu mipango ya kupindua Serikali.

Shtaka la nne, Odinga na Otieno Mak’onyango (aliyekuwa mbunge wa Alego Usonga), Julai 31 1982, walikwenda katika Baa ya Mausoleum iliyoko Buru Buru Estate jijini Nairobi, kujadili mipango ya kupindua Serikali, walikuwa na Ochuka na watumishi wengine kutoka KAF.

Odinga na Mak’onyango Julai 31 1982, walikwenda Baa ya Ongere na Shaurimoyo jijini Nairobi kwa madhumuni ya kuwasiliana na Ochuka na askari wengine wa KAF kabla ya kuanza mpango wa kupindua Serikali usiku huo.

Katika shtaka la sita, kiongozi wa ODM na mbunge huyo, usiku wa Julai 31 na Agosti 1 1982, walivamia nyumba ya Alfred Vincent Otieno katika Barabara ya Ngong jijini Nairobi na kumsaidia Ochuka na wanajeshi wengine kutumia nyumba hiyo kama kituo cha operesheni katika mipango yao ya kupindua Serikali.

Odinga na mtu mwingine aliyeitwa Opwapo walishutumiwa kuwa, usiku walipeleka taa na betri mbili kwenye nyumba ya Alfred Vincent Otieno katika Barabara ya Ngong jijini Nairobi kwa ajili ya matumizi ya mapinduzi.

Shtaka la nane kati ya Julai 31 na Agosti 1, 1982, Odinga alitoa gari lake aina ya ‘Peugeot 504’ lenye namba za usajili KVZ 642 na kuwapa Ochuka na Sajenti Joseph Ogidi Obuon ili kuwawezesha kuchukua gari lingine la SSE Land Rover kwa ajili ya matumizi ya kupindua Serikali.

Agosti 1, 1982, ilidaiwa kuwa Odinga alitoa gari aina ya Peugeot 305 iliyokuwa ya rafiki wa familia yake na kumpatia Ochuka na wengine ili kupindua Serikali.

Agosti 9 1982, Odinga alizuru nyumba ya Otieno katika Barabara ya Ngong Nairobi na kuondoa meza iliyotumiwa na waasi wakati wa kujaribu kujenga nyumba hiyo kama kituo cha kutekeleza mapinduzi.

Muda mfupi baadaye, Odinga, Alfred Otieno na Mak’onyango walifikishwa mahakamani.

Wakati kesi ikiendelea, jina la Jaramogi Oginga Odinga ambaye ni baba mzazi wa Raila Odinga, lilitajwa mara kadhaa mahakamani kuwa ndiye aliyefadhili mpango huo, na aliwekwa chini ya kifungo cha nje kwa miezi kadhaa.

Odinga mwenyewe aliwekwa kizuizini kwa miaka sita na aliachiwa Februari 1988 lakini akawekwa kizuizini tena Agosti mwaka huo hadi Juni 1989. Wakati wenzake wanakamatwa Kenya kwa mpango wa mapinduzi aliouanzisha, Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu walikuwa Tanzania walikokimbilia na kupewa hifadhi ya kisiasa.

Julai 9, 1987, wote wawili walinyongwa katika Gereza la Kamiti mjini Nairobi.

Waliondokaje Tanzania hadi walipokutana na vifo kwa kunyongwa? Usikose kesho.