Rais mpya aapishwa Namibia, achukua nafasi ya Geingob

Rais mpya Namibia,Nangolo Mbumba akiapishwa kuchukua nafasi ya Rais Hage Geingob aliyefariki dunia leo Februari 4, 2024

Muktasari:

  • Rais mpya, Nangolo Mbumba pamoja na makamu wake, Netumbo Nandi-Ndaitwah wataiongoza Serikali ya Namibia hadi mwishoni mwa mwaka huu ambapo Taifa hilo litafanya uchaguzi mkuu.

Windhoek. Makamu wa Rais wa zamani wa Namibia, Nangolo Mbumba ameapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa hilo, akichukua nafasi ya Hage Geingob aliyefariki dunia leo Februari 4, 2024 akiwa hospitali.

Kwa mujibu wa AFP, Mbumba ameapishwa sambamba na Makamu wa Rais mpya, Netumbo Nandi-Ndaitwah ambaye kabla ya kiapo hicho alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa Namibia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wawili hao watatumikia nafasi zao hadi mwisho wa mwaka ambapo utafanyika uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge nchini humo.

Mbumba, aliyezaliwa Agosti 15, 1941, alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Namibia tangu 2018. Mwanachama huyo aliyejitoa kwa chama chake cha Swapo, anajivunia uzoefu wake wa kuongoza wizara mbalimbali nchini Namibia. .

Nyadhifa zake za huko nyuma ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Maji na Maendeleo Vijijini (1993-1996), Waziri wa Fedha (1996-2003), Waziri wa Habari na Utangazaji (2003-2005), Waziri wa Elimu (2005-2010), na Waziri wa Usalama (2010-2012).

Kuanzia 2012 hadi 2017, Mbumba alishika wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama tawala cha Swapo.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Namibia leo Jumapili, Februari 4, 2024, Mbumba amesema, “Ni kwa huzuni na masikitiko makubwa kwamba ninawajulisha kuwa mpendwa wetu, Dk Hage Geingob, Rais wa Jamhuri ya Namibia, amefariki dunia leo katika Hospitali ya Lady Pohamba ambako alipokuwa akipata matibabu.”

Geingob, Waziri Mkuu wa kwanza na Rais wa tatu wa Namibia, alipitia safari ya ajabu kutoka kuwa mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi hadi kuwa mwanasiasa mwenye sifa kubwa katika maisha yake yote.

Geingob (82) aliapishwa kuwa Rais wa Namibia Machi 21, 2015, na alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka mitano mwaka 2019. Amehudumu kama Waziri Mkuu kuanzia 1990-2002 na 2012-2015, pamoja na majukumu mengine muhimu ya uwaziri na uongozi.

“Timu yake ya matibabu imekuwa ikijaribu kila iwezalo kuhakikisha kuwa Rais wetu anapona,” Mbumba amesema katika taarifa hiyo. “Inasikitisha, licha ya juhudi za dhati za timu kuokoa maisha yake, cha kusikitisha, wananchi wenzangu, Rais Geingob alifariki dunia.”

“Taifa la Namibia limepoteza mtumishi mashuhuri wa watu, mwanasiasa maarufu wa mapambano ya ukombozi, mbunifu mkuu wa katiba yetu na nguzo ya Namibia,” imeeleza taarifa hiyo ya Mbumba.

Januari 19, 2024, Rais wa Namibia alisema timu ya matibabu ya Geingob iligundua kiongozi huyo ana seli za saratani.