Sh2.2 bilioni kupiga jeki uzalishaji wa mirungi

Muktasari:
- Inaelezwa kwamba, mbali na kusaidia vyama viwili vya ushirika vya Meru na Embu katika kuwakinga wakulima wa miraa dhidi ya kupanda kwa gharama za uzalishaji, uimarishaji wa sera za miraa utasaidia kuliendeleza zo hilo na hivyo kuingiza Zaidi mapato ya kigeni.
Nairobi. Wakati Tanzania mirungi (miraa) ni haramu, Serikali ya Kenya imedhamiria kukiendeleza kilimo hicho kwa kuwekeza Sh130 milioni pesa za nchi hiyo kwaajili ya miundombinu ya umwagiliaji na uendelezaji masoko. Mtandao wa Taifa Letu umeripoti.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo wa nchi hiyo, Mithika Linturi, fedha hizo ambazo ni sawa na Sh2.2 bilioni za Tanzania, mgao huo utasaidia kuimarisha vyanzo vya maji na uboreshaji wa masoko katika maeneo yanayolima mirungi.
Ili kuhakikisha wakuzaji wanapata maji ya kutosha kwaajili ya kilimo hicho kinachoshika kasi nchini humo, Waziri Linturi amesema: “Pesa hizo zitatumika kujenga mabwawa ili yapatikane maji ya kumwagilia miraa na hivyo kuondokana na kilimo tegemezi kwa mvua.”
Waziri huyo mwenye dhamana ya Kilimo nchini humo, ameagiza Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) kushirikiana na Taasisi ya Miraa ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru ili kuibua mikakati madhubuti ya kuongeza thamani kwa zao hilo.
“Miraa ilileta pato la Sh6 bilioni mwaka 2022. Serikali imekuwa ikipiga jeki juhudi za uimarishaji wa zao la miraa tangu mwaka 2013 na hadi kufikia sasa, Sh344 milioni zimetumika kuimarisha vibanda vya miraa, vyanzo vya maji na uchimbaji mabwawa. Serikali ya Kenya Kwanza imejitolea kuhakikisha ukuzaji wa miraa unaimarika,” amesema Linturi.
Inaelezwa kwamba, mbali na kusaidia vyama viwili vya ushirika vya Meru na Embu katika kuwakinga wakulima wa miraa dhidi ya kupanda kwa gharama za uzalishaji, uimarishaji wa sera za miraa utasaidia kuliendeleza zo hilo na hivyo kuingiza Zaidi mapato ya kigeni.
Waziri Linturi amesema kilimo cha mirungi kimeongeza maradufu tangu mwaka 2019 hadi 2023.
Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Mirungi Nyambene (Nyamita), Kimathi Munjuri amefurahia hatua ya serikali kutoa fedha hizo kwa sekta ndogo ya kilimo cha mirungi kwa kuwa serikali ilikuwa imesitisha ufadhili mwaka 2020.
Mwaka 2016, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza kutenga dola za Kimarekani 10 milioni kwa ajili ya kusaidia wakulima wa mirungi wakati akitia saini mswada unaotambua mirungi kuwa mmea wa kulizalishia taifa mapato ili uwe sheria.
Pia Rais Kenyatta alitangaza nia ya kuunda jopo kazi la kuangazia changamoto zinazokabili sekta ya ukuzaji wa mirungi ambayo itatoa mapendekezo kwa serikali.
Msaada huo ulikuja wakati baadhi ya nchi Ulaya na kwingineko, kupiga marufuku uuzaji wa mmea huo.