Wawili mbaroni wakidaiwa kusafirisha mirungi

Muktasari:
- Watuhumiwa hao ambao ni Halid Salimu Awadhi (54) dereva mkazi wa Temeke na Yusuph Kondo (46) fundi mkazi wa Bungoni, walikamatwa na mirungi bunda 184 sawa na Kilo 61, ambayo walikuwa wakiisafirisha kwa gari lenye namba za usajili T 258 CJB Toyota X-Trail.
Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linawashikilia watu wawili wakazi wa Dar es Salaam, kwa tuhuma za kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni mirungi bunda 184 sawa na Kilo 61.
Akizungumza leo Jumatano Aprili 5, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa watu hao April 1, 2023 saa 7:20 mchana katika eneo la Mengwe wilayani Rombo.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Halid Salimu Awadhi (54) dereva mkazi wa Temeke na Yusuph Kondo (46) fundi mkazi wa Bungoni, Dar es Salaam ambapo walikiwa wakisafirisha mirungi hiyo kwa Gari lenye namba za usajili T258 CJB, Toyota X-Trail rangi ya Silver.
"Watuhumiwa hao ambao wote ni wakazi wa Dar es Salasm, wakitumia gari aina ya Toyota X Trail, walipofika kizuizi cha polisi Mengwe, walipekuliwa na kukutwa na mirungi bunda 184 sawa na kilo 61."
Aidha Kamanda Maigwa amesema, watuhumiwa hao, watafikishwa mahakamani wakati wowote.