Suminwa Waziri Mkuu mpya DR Congo
Muktasari:
- Suminwa ameteuliwa akichukua nafasi ya Jean-Michel Sama Lukonde aliyejiuzulu wiki mbili zilizopita.
Kinshasa. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi leo Aprili mosi 2024 amemteua Waziri wake wa Mipango, Judith Tuluka Suminwa kuwa waziri mkuu.
Suminwa anakuwa mwanamke wa kwanza kwa Taifa hilo kuwa na Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Jean-Michel Sama Lukonde aliyejiuzulu wiki mbili zilizopita.
Lukonde (46), aliyekuwa madarakani kwa miaka mitatu, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu Februari 15, 2021 baada ya muungano wa Rais wa zamani, Joseph Kabila na ule wa Félix Tshisekedi kuvunjika
Uteuzi wa Suminwa sasa unamaliza utata wa Serikali yake iliyorudi madarakani baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 20, 2023 na kumpa ushindi.
Tshisekedi alikuwa akitafuta kuungwa mkono bungeni na vyama vingine vyenye wabunge wengi kabla ya kuteua waziri mkuu na kuunda serikali.
"Naelewa makujumu makubwa tuliyonayo... tutafanya kazi kwa ajili ya amani na maendeleo ya nchi," amesema Suminwa kupitia televisheni ya taifa hilo akinukuliwa na Reuters.
Utawala wa nchi hiyo unakabiliwa na changamoto ya migogoro na majanga ya kibinadamu upande wa mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Katika kampeni za uchaguzi, Rais Tshisekedi aliahidi kupambana na rushwa, kujenga upya uchumi, kupambana na kutokuwa na usawa na migogoro ya mashariki ya nchi hiyo, hata hivyo wachambuzi wanasema ameshaanza kufeli katika ahadi zake.
Wanahoji, Suminwa ambaye ni msomi kutoka Chuo kikuu cha Free cha Brussels ataweza kupambana kutekeleza ahadi hizo?