Waafrika 29 wazama baharini wakitorokea Italia

Katika mwendelezo wa wimbi la wahamiaji kutoka barani frika kwenda Ulaya kutafuta maisha bora, takribani watu 29 wamefariki dunia walipokua wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kutoka nchini Tunisia kuelekea Italia baada ya boti mbili walizokuwa wakisafiria kuzama baharini.
Tunisia. Takriban wahamiaji 29 wamekufa baada ya boti mbili kuzama katika pwani ya Tunisia, maafisa wanasema.
Wahamiaji hao wa kusini mwa jangwa la Sahara walikuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuingia nchini Italia.
Hii ni mwendelezo wa boti za wahamiaji kupinduka katika pwani ya Tunisia katika siku chache zilizopita, na nyingine tano kuzama katika siku nne zilizopita.
Haya yanajiri baada ya Tunisia kuanzisha kampeni dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika wasio na vibali.
Wakati huo huo, maofisa wa Italia katika Kisiwa cha Lampedusa wanasema wamezidiwa, baada ya rekodi ya wahamiaji 2,500 kuwasili katika saa 24 zilizopita.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni ameonya kuwa Ulaya iko hatarini kuona wimbi kubwa la wakimbizi wakiwasili kwenye nchi zake.
Tunisia imekuwa kinara wahamiaji wanaotaka kufika Ulaya, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionyesha wahamiaji wasiopungua 12,000 waliotua katika Italia mwaka huu wametoka Tunisia. Idadi hiyo ilikuwa 1,300 tu katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Hata hivyo, walinzi wa pwani ya Tunisia wanasema wanachukua hatua kusimamisha vivuko vya wahamiaji, baada ya kusimamisha karibu meli 80 zilizokuwa zikielekea Ulaya katika siku nne zilizopita, kulingana na Shirika la Habari la Reuters.
Katika hotuba yenye utata mwezi uliopita, Rais wa Tunisia aliwashutumu wahamiaji wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaoishi nchini humo kwa kusababisha wimbi la uhalifu na kuwataja kuwa tishio la idadi ya watu.
Maoni ya Kais Saied yalishutumiwa vikali na Umoja wa Afrika na kulaaniwa kama "hotuba ya chuki ya kibaguzi" na mashirika ya haki za binadamu.
Maoni haya yamewaacha baadhi ya Waafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara nchini Tunisia wakiishi kwa hofu, huku baadhi wakisema wameshuhudia ongezeko la matukio ya kibaguzi.
Hii imesababisha baadhi ya nchi, kama Ivory Coast na Guinea, kuwarejesha makwao raia wao kutokana na kuongezeka kwa hali ya kutovumiliana nchini Tunisia.
Uchumi wa Tunisia uko katika hali mbaya, na unakabiliwa na mgogoro baada ya mazungumzo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kukwama.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken pia ameonya kwamba Tunisia inahitaji haraka kufikia makubaliano ya uokoaji na IMF.
Imeandaliwa na Victor Tullo