Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

30 mbaroni wakidaiwa kughushi mafao NSSF

Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Watuhumiwa wanadaiwa kukamatwa na nyaraka bandia zinazohusu kuacha kazi, vyeti vya huduma, taarifa za uongo za ugonjwa, hati za uongo za kufukuzwa kazi na fomu za kugushi za kuomba mafao ya NSSF.

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imewakamata watu 30 kwa tuhuma za kughushi nyaraka zinazohusiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa lengo la kujipatia malipo ya mafao kwa njia ya udanganyifu kutoka mfuko huo.

Idadi hiyo ya watuhumiwa imerekodiwa katika kipindi cha miezi minne kuanzia Desemba 2023 hadi Aprili 2024, wote wakituhumiwa kufanya njama za kujipatia fedha kutoka mfuko huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 9, 2024 na Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro, watuhumiwa wamekamatwa na nyaraka bandia zinazohusu kuacha kazi, vyeti vya huduma, taarifa za uongo za ugonjwa, hati za uongo za kufukuzwa kazi na fomu za kugushi za kuomba mafao ya NSSF.

Amewatajwa waliokamatwa kuwa ni Diocress Kahwa (35) mkazi wa Mbezi, mwalimu wa Shule ya Msingi Maxmilian ya Segerea; Barnabas Bonivencha na wenzake 11 wa kampuni binafsi ya ulinzi ya G4S wanaodaiwa kuwasilisha taarifa za uongo za kuacha kazi ili wapate mafao wakati bado wapo kazini.

Mwingine ni Carolina Mushi (37), mkazi wa Upanga, mtumishi wa Benki ya Stanbink anayetuhumiwa kughushi taarifa za hospitali za ugonjwa ili apate fao la matibabu.

Katika tuhuma hizo, Carolina ameunganishwa na Gregory Rweikiza (44), mkazi wa Goba anayetuhumiwa kusuka mpango wa kughushi taarifa hizo.

Wamo pia Michael Mpogolo (38) na Sabato Thomas (27), wakazi wa Madale Mivumoni, Dar es Salaam wanaotuhumiwa kughushi nyaraka za wafanyakazi wawili waliofariki dunia (Servas Tesha na Korodias Shoo) waliokuwa wanafanya kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa watafikishwa makahamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Amewataka watu waache tabia ya udanganyifu na kughushi nyaraka akisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.


Makosa ya usalama barabarani

Wakati huohuo, Kamanda Muliro amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024, takwimu za makosa ya usalama barabarani ndani ya Kanda Maalumu ya Dar es Salaam zinaonyesha jumla ya makosa 221,724.

Kati ya hayo, amesema yanayohusu magari yalikuwa 173,190 na makosa ya pikipiki yalikuwa 48,534.

Amesema wahusika walichukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini za papo kwa hapo na baadhi ya madereva na wapanda pikipiki walifikishwa mahakamani.

Kamanda Muliro amesema madereva wa pikipiki na magari 89 wamefikishwa mahakamani, 60 walikutwa na kosa la ulevi na walitozwa faini, 759 walikamatwa kwa kosa la kupita kwenye taa nyekundu.

Amesema madereva wa pikipiki waliokamatwa kwa kuzidisha abiria (mishikaki) ni 3,779, huku makosa mengine yakiwa 217,034.


Sherehe za Eid el Fitr

Akizungumzia sherehe za Eid el Fitr ambazo zinatarajiwa kuadhimishwe kesho Aprili 10 au Aprili 11, 2024 amewataka madereva wa vyombo vya moto kutotumia vileo wakati wa kuedesha magari au pikipiki.

Pia wazazi na walezi wamekumbushwa kuepuka kuwaacha watoto wadogo watoke peke yao barabarani na maeneo mengine.

Kamanda Muliro amesema wamejipanga kuhakikisha usalama unaimarishwa katika maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam, zikiwemo nyumba za ibada, mitaani, fukwe za bahari na katika makazi ya watu.