Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo sita yaliyotikisa mafao Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imesema changamoto inayolalamikiwa na baadhi ya wastaafu haihitaji mabadiliko ya sheria wala kanuni bali wastaafu kuelewana na mifuko husika ili iwaongezee muda wa marejesho ya mkopo.

 

Dar es Salaam. Ni wazi kuwa kanuni mpya za Sheria ya Hifadhi ya Mifuko ya Jamii ya mwaka 2018 zimeibua maswali mengi kwa wananchi.

Mathalani, wapo wanaohoji juu ya sababu za kupunguzwa kwa ulipwaji wa mafao kutoka asilimia 50 mpaka 25 kwa mkupuo.

Pia, wapo wanaohoji kiasi cha fedha kurejea serikalini baada ya mstaafu kufariki dunia, ikiwa ni baada ya wategemezi wake kulipwa mafao yake ya miaka mitatu.

Wengine wanahoji kuhusu kujitoa licha ya ukweli kuwa hakuna aina hiyo ya mafao. Baadhi wanajiuliza kwa kanuni hizo, nani atapata na nani atakosa kati ya watumishi wa sekta binafsi na serikalini. Pia, kuna wanaohoji baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii watapataje mafao yao ikiwa walichangia katika mifuko miwili tofauti.

Wanaodai mafao yao wamebaki na sintofahamu juu ya malipo yao kama yatafanyika kwa kutumia kanuni na sheria ya zamani au mpya.

Sababu kupunguzwa

mafao ya mkupuo

Akijibu maswali hayo juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka alisema ukokotoaji huo si mpya kwani ulianza tangu mwaka 2014 kwa mifuko yote isipokuwa kwa wanachama wa PSPF, GEPF na LAPF wa kabla ya Julai Mosi 2014. Lakini sasa lengo ni kuweka usawa kikokotoo miongoni mwa wanachama ili wawe wanachangia kwa kiwango kipya.

“Licha ya kuwa wanachama wote wa mifuko wanachangia asilimia 20 ya mshahara, lakini mafao ya mkupuo yalikuwa yanatofautiana kulingana na mfuko anaotumia. Baada ya tathmini tulikuja na kikokotoo ambacho kinaweza kuboresha mafao ya wanachama na kuimarisha sekta ya mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema Isaka.

Kwa mabadiliko ya sasa, wanachama wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii watakuwa wakipewa mafao mkupuo kwa asilimia 25 tofauti na awali ambako wale wa mifuko ya watumishi wa umma walikuwa wakipewa mafao ya mkupuo ya asilimia 50.

Miaka mitatu mstaafu

akifariki

Isaka alisema mifuko ya hifadhi ya jamii utaratibu wake ni kama wa bima kwamba watu wanakusanya pamoja lakini fedha anapewa mwenye uhitaji kwa wakati huo ndiyo maana kuna wanaopata pensheni kwa miaka 28 na wengine mwaka mmoja tu.

“Baada kupata mafao ya mkupuo ambayo ni asilimia 25, mstaafu ataendelea kulipwa asilimia 75 ya pensheni ambayo itagawanywa kwa kila mwezi kwa kipindi chote cha maisha yake na atakapofariki familia yake itapata pensheni ya miezi 36 (miaka mitatu),” alisema Isaka akitoa mfano wa mtumishi ambaye mshahara wake wa mwezi ni Sh442,000 kwamba endapo atachangia kwa miaka 32, jumla ya michango yake itakuwa Sh8.64 milioni, lakini mafao yake ya mkupuo yatakuwa Sh10.81 milioni na kila mwezi atakuwa akilipwa Sh216, 293 maisha yake yote, na akifa familia yake itapata Sh7.78 milioni (pensheni ya miezi 36) hata kama atakuwa amelipwa pensheni kwa miaka 20 au zaidi.

Nani anapata/anapoteza

Kulingana na maelezo ya SSRA, hakuna mtu anayepoteza, lakini wanachama wa LAPF, GEPF na PSPF ambao awali walikuwa wanapata mafao ya mkupuo ya asilimia 50, sasa mkupuo wao utapungua kwa asilimia 25 (nusu) lakini pensheni yao ya kila mwezi itaongezeka.

“Kiwango kilichopunguzwa hapo ni mkupuo tu. Fedha zake zimeongezwa kwenye pensheni ya kila mwezi. Bado tunawalinda watu wenye kikokotoo kikubwa, kwa wanachama wa PSSSF bado kikokotoo chao ni 1/540 na wanauza wastani wa kuishi 15.5,” alisema.

Alisema malalamiko yaliyopo yanatokana na watu wachache waliokuwa na mikopo ya nyumba kwa kuwa wakati PSPF ikitoa mkupuo wa asilimia 50 mwanachama alikuwa anaruhusiwa kukopa nyumba hadi asilimia 25 ya mkupuo wake. Alishauri wanachama hao washauriane na mifuko yao, lakini si kubadilisha sheria wala kanuni.

Mifuko tofauti

Isaka alisema kabla ya kuunganishwa kwa mifuko na kuundwa kwa kanuni hizi, wanachama wa LAPF, GEPF na PSPF walikuwa wanatumia kikokotoo cha asilimia 50 hata baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii mwaka 2014.

Isaka alisema waliokuwa wanatumia mifuko tofauti, sasa watatumia mfuko mmoja na amana zao zitaunganishwa kwa kuwa sasa kuna mifuko miwili tu; wa sekta ya umma na binafsi. Kuhusu madeni ya Serikali katika mifuko hiyo, Isaka alisema Serikali haijakopa katika sekta ya mifuko ya hifadhi ya jamii tangu mwaka 2013 kwa sababu tayari ilifikia ukomo ambao ni asilimia 10 kwa mujibu wa mwongozo.

“Kwenye vitabu vya Serikali, madeni yake kwa mifuko ya hifadhi ya jamii bado yapo mnaweza kupata ufafanuzi zaidi kwa wenye dhamana. Bado Serikali haijakana madeni yake na mara ya mwisho ilisema itatoa hati fungani ili kulipa hayo madeni yake” alisema.

Kuhusu kujitoa

Mwanasheria wa SSRA, Onorius Njole alisema hakuna kitu kinaitwa fao la kujitoa na gharama yake ni kubwa kwani mtu anayefanya hivyo, anarejeshewa michango yake tu na akistaafu hakutakuwa na pensheni ya kila mwezi na atakaporejea katika kuchangia ataanza upya.

“Watu wanajitoa kwa sababu mtu amekosa kazi na hana namna ya kufanya baada ya kupoteza ajira ndiyo maana likaanzishwa fao jipya la kukosa ajira . Mwanachama kama hajaacha kwa hiari yake, mfuko utampatia pensheni ya asilimia 33.3 ya mshahara wake wa mwisho kwa miezi sita,” alisema.

Endapo atapata ajira, alisema mwanachama atarudi tena katika utaratibu wa kawaida na hiyo pensheni yake haitakatwa katika mafao yake ya mwisho.

“Fao la kujitoa liliondolewa likaletwa hilo lenye masilahi makubwa kwa wanachama.”