Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baba jela miaka 30 kwa kumnajisi mwanawe kwa miaka mitatu

Muktasari:

 Baba afungwa miaka miaka 30 jela kwa kuzini na mtoto wake. Imeelezwa kuwa ndiye aliyemtoa bikira mwaka 2020 na akaendelea kuzini naye hadi mwaka jana alipokamatwa akiishi naye kama mke. Ushahidi uliotolewa na mtoto pamoja na mama yake, ulithibitisha kitendo hicho pasi na shaka.

Geita. Ni zaidi ya maajabu. Ndivyo unavyoweza  kuelezea kitendo cha mkazi wa wilaya ya Chato, kumgeuza mwanawe wa kumzaa kama mke na kuzini naye kisha kumvunja ungo wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Kevin Mhina, amebariki kifungo cha miaka 30 jela alichopewa mwanaume huyo ambaye alizini na mwanae huyo mwenye umri wa zaidi ya miaka 12, kwa kipindi cha miaka 3.

Mahakama Kuu ya Tanzania katika kushughulikia kesi hiyo ilihifadhi jina la mtoto na kumpa jina lenye kifupisho cha ‘ASR’ ili kumlinda na ni sababu hizo hizo, gazeti hili halitataja jina la baba yake gazetini ili kuepuka kumtambulisha kwa Jamii.


Baba alivyotekeleza ukatili

Katika ushahidi wake, mtoto huyo alisema siku moja na mwezi asioukumbuka mwaka 2020, baba yake ambaye walikuwa wakiishi wote kijiji cha Katale, alimchukua na kumpeleka Chato Msilale kwa ajili ya kumunulia sare za shule.

Siku hiyo waliishia kufikia katika nyumba ya babu yake ambako walilala chumba kimoja na baba yake, huku baba akilala chini kwenye gunia na yeye akilala na watoto wengine kwenye godogo na usiku alihisi mtu anamshika kwenye miguu.

Kwa mujibu wa ushahidi wake huo, aligundua ni baba yake na hapo hapo baba akimuonya asije akamwambia mtu yeyote, ndipo baba yake hiyo akamchukua hadi kwenye gunia, akamvua nguo na kumzini, kitendo kilichompa maumivu.

Kulingana na ushahidi, tangu usiku huo, ikawa ndio mchezo wa baba kumbaka mwanae kwani siku iliyofuata, baba yake huyo alimbaka tena ambapo mtoto alilalamika kwa bibi yake ambaye aliyeitisha kikao na kumfukuza mrufani huyo.

Mtoto akaendelea kukaa na bibi yake mpaka baba yake alipoamua kwenda kumchukua na kwenda naye kijiji cha Nyambiti na baadae kijiji cha Katoro katika nyumba ya kupanga walikoishi kama familia yeye, baba yake na mama wa kambo.

Pia alikuwepo kaka yake ambaye ni mtoto wa mama huyo wa kambo aliyeishi na baba yake na huko nako kulingana na ushahidi, baba yake alimbaka mara tatu.

Katika ushahidi wake huo kortini, mtoto alisimulia kuwa walipohamia kijiji cha Nywalwambu, baba yake aliendelea kuzini naye usiku na siku moja katika mwezi wa Ramadhan alizini naye na  alipoteza urijali wake (alipoteza bikira).

Damu zilikuwa zinatoka kutoka kwenye uke wake ambapo baba yake alimwambia aende kuoga ili kufuta damu hizo ambapo baadae walihamia Biharamulo ambapo baba yake alijenga nyumba ya kuishi katika eneo lililokuwa na rafiki yake,

Mrufani akamwambia aende kulala eneo mojawapo ambalo kulikuwa na kipande kimoja tu cha shuka sakafuni ambapo baadae baba yake huyo aliingia katika chumba hicho usiku na kumuamsha ambalo alizini naye hapo sakafuni.

Aliendelea kueleza kuwa, baba yake alipooa walirudi kwa bibi yake eneo la Katale na Agosti 27,2023 akiwa usingizini, bibi yake alisikia kama mtu amefungua mlango na akauliza ni nani alikuwa ameingia nyumbani ambapo mtu huyo alikimbia.

Siku iliyofuata, baba yake aliingia chumbani akiwa na dawa ya kienyeji na kumwambia mtoto ilikuwa ni kwa ajili ya meno, mrufani alipaka dawa hiyo kwenye mwili wake (baba) akiwa uchi wa mnyama na kisha akambaka mtoto.

Bibi yake alitilia mashaka ambapo alimuuliza mtoto kama aliona mtu yoyote wenye chumba chake lakini hakumwambia chochote ila baadae mrufani (baba) alirudi tena na kumchukua hadi kitandani ambako alimbaka na kuondoka.

Hapo mtoto ndio akaamua kutoa taarifa kwa shangazi yake ambaye hata hivyo hakuchukua hatua yoyote, akaamua kwenda kwa mwenyekiti wa kitongoji na baadae akamrudia shangazi yake naye aliamua kumshirikisha mama wa kambo.

Kwa pamoja waliamua kutoa taarifa kituo cha Polisi cha Buzirayombe ambapo mhalifu huyo alikamatwa na mwathirika akapelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi na daktari akaingiza vidole viwili vikazama ndani sentimeta 6.


Ushahidi wa mke, dada

Katika ushahidi wake, mke wa mfungwa huyo ambaye ni mama wa kambo wa mtoto huyo, alieleza kuwa yeye katika siku tofauti tofauti, alibaini mumewe huyo akitokea kutoka kwenye chumba cha mwanae usiku wa manane.

Kabla ya mtoto kuvijisha jambo hilo, mkewe alisema tayari alikuwa ameshaanza kushuku kwamba mumewe alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mtoto na alimuuliza mumewe siku moja akitokea chumbani kwa mtoto lakini alikanusha.

Ushahidi wa dada wa mrufani haukutofautiana na ule wa wifi yake na alieleza namna mtoto alivyofika kwake na kumweleza juu ya kile anachofanyiwa na baba yake na ni yeye aliamua kumshirikisha wifi yake wakaamua kuchukua hatua.

Ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni Ofisa wa Polisi, alielezea kuwa yeye ndiye alimpokea mtuhumiwa kituo cha polisi na kuandika maelezo yake ya onyo na pia akaandika maelezo ya daktari akieleza namna alivyobaini mtoto sio bikira.

Katika utetezi wake, mrufani alikiri kwamba yeye ni baba mzazi wa mwathirika na kwamba ni binti yake lakini akakana ushahidi wa kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanae na kwamba ushahidi dhidi yake ulikuwa ni wa kutengeneza.

Aliiomba mahakama isiuamini ushahidi wa mkewe kwa kuwa ana uhusiano wa karibu na dada yake ambaye ni wifi kwa mkewe na kudai kwamba alilazimisha kuandika maelezo.

Mwisho wa kesi hiyo katika mahakama ya wilaya ya Chato, mahakama hiyo ilimuona ana hatia ya kosa hilo la kufanya mapenzi na maharimu (incest by male) na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, akakata rufaa lakini Jaji Mhina akaitupilia mbali.


Hukumu ya jaji ilivyokuwa

Kulingana na hukumu ya Jaji Mhina aliyoitoa leo Aprili 3,2024, alisema anakubaliana na uamuzi wa mahakama ya wilaya ya Chato wa kumtia hatiani mzazi huyo na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela ambacho naye anakibariki kuwa anastahili.

Jaji Mhina alitoa hukumu hiyo wakati akitoa hukumu ya rufaa ya mrufani huyo aliyekuwa akipinga adhabu hiyo, ambapo alisema upande wa Jamhuri uliweza kuthibitisha shitaka hilo bila kuacha mashaka na hana sababu ya kuitengua.

Kuthibitisha kama mtoto aliingiliwa, Jaji alisema ushahidi bora ni wa mwathirika ambaye katika kesi hiyo mtoto mwenyewe alitoa ushahidi kama shahidi wa kwanza na ushahidi wake na ulithibitisha baba kumwingilia kwa miaka mitatu.

“Ushahidi wa mtoto ulithibitisha kwamba (rufani) alimbaka mwanae kwa kipindi cha miaka mitatu. Hati ya mashitaka ilionyesha alimwingilia mwanae wa kumzaa kuanzia mwaka 2020 hadi Agosti 2023,” alisema Jaji Mhina katika hukumu yake.

“Zaidi katika ushahidi wa daktari alimfanyia uchunguzi mwathirika (mtoto) alimkuta hana bikira na vidole vyake viwili viliingia kwenye sehemu za siri za mtoto kama sentimeta sita na iliungwa mkono na PF3 (fomu ya Polisi),” alisema.

“Kwa hiyo hakuna ubishi kuwa mwathirika ana umri wa miaka 12 aliingiliwa. Lakini hata ushahidi ambao hauna mashaka ni mrufani ndiye alikuwa akimwingilia. Kwa hiyo kosa la kuzini na maharimu lilithibitishwa,”alisisitiza Jaji Mhina katika hukumu yake.

Pamoja na uchambuzi huo, lakini Jaji Mhina alizitupa sababu zote 7 za rufaa alizokuwa ameziwasilisha mahakamani kupinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela na kusema anakubaliana na kile ambacho Hakimu wa Mahakama ya wilaya Chato alikibaini.

“Shitaka la kufanya mapenzi na maharimu dhidi ya mrufani lilithibitika pasipo kuacha mashaka. Mrufani alikuwa akizini na mwathirika akiwa anajua kuwa ni mtoto wake wa kibiolojia (biological father). Sina mashaka na kile mahakama ilichokibaini,” alisema.

Jaji akasema anabariki kifungo cha miaka 30 alichohukumiwa na mahakama ya chini (wilaya ya Chato) kwamba ana hatia na hukumu aliyopewa ilikuwa ni sahihi.