‘Chanjo ya kuzuia saratani mlango wa kizazi haizuii mimba’

Mganga mkuu wa Mkoa wa Arusha (RMO), Dk Silvia Mamkwe

Muktasari:

Jamii nchini imeaswa kuachana na dhana potofu kuwa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 inazuia ujauzito.

Arusha. Mganga Mkuu wa Mkoa Arusha (RMO), Dk Silvia Mamkwe ameitaka jamii iachane na dhana potofu kuwa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV) inayotolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 inazuia ujauzito.

Dk Mamkwe ameyasema hayo kwenye semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa kanda ya kaskazini juu ya kuandika habari za chanjo iliyoandaliwa na Wizara ya Afya na kufanyika jijini Arusha.

Ameeleza kuwa jamii inapaswa kuhakikisha wasichana wenye umri wa miaka 14 wanapatiwa chanjo hiyo kwa awamu mbili kwa kuchanjwa mara moja na baada ya miezi sita anamalizia kwani haizuii ujauzito.

"Hiyo ni dhana potofu inayoenezwa kuwa chanjo hiyo inazuia ujauzito pindi wasichana wakipatiwa hivyo washiriki kwa manufaa yao kwani inazuia saratani ya mlango wa kizazi," amesema Dk Mamkwe.

Amesema hakuna haja kwa jamii na watoto wa kike kuogopa kupata chanjo hiyo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi sababu ni moja ya saratani inayotibika na kuepukana na kifo.

"Chanjo hii ni muhimu kwani katika saratani ambazo zinatibika ni hii ya saratani ya mlango wa kizazi na serikali imewekeza nguvu kubwa hivyo jamii iachane na dhana potofu," amesema Dk Mamkwe.

Meneja wa mpango wa Taifa wa chanjo, Dk Florian Tinuga amesema hakuna chanjo inayoingizwa nchini na Serikali yenye matatizo hivyo jamii ishiriki katika chanjo zote bila hofu.

Dk Tinuga amesema kabla ya kuanza kutumika nchini, wataalamu huwa wanapitia ipasavyo na kukagua chanjo zote zinazoelekezwa na Wizara ya Afya.

Ofisa mpango wa Taifa wa chanjo Wizara ya Afya, Lotalis Gadau amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa waandishi wa habari wa kanda tofauti nchini ili kuwaongezea uelewa wa kuandika habari za chanjo.

Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications LTD wa Mkoa wa Tanga, Raisa Said amesema semina hiyo iliyowashirikisha waandishi wa habari wa mikoa ya Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Arusha, itawajengea uwezo zaidi wa kuandika habari za chanjo.