Dk Kijaji anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kilele cha kumlinda mlaji

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
Leo Machi 13, FCC ilikuwa na kliniki ya kusikiliza changamoto za mlaji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji iliyoanza kuadhimishwa Machi 8, 2024 na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 15, 2024
Dar es Salaam. Wakati kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji kikifanyika Machi 15 mwaka huu, Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk Ashantu Kijaji anatarajia kuwa mgeni rasmi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), William Erio amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Leo Machi 13, FCC ilikuwa na kliniki ya kusikiliza changamoto za mlaji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumlinda Mlaji iliyoanza kuadhimishwa Machi 8, 2024 na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 15, 2024.
Kliniki hiyo iliendeshwa katika ofisi za FCC Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Erio amesema wakati wa kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Hoteli ya Protea kutakuwa na kongamano litakalohusisha wadau wa sekta kuhusu akili nemba.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2024 inasema: “Matumizi ya akili nemba yanayozingatia haki na uwajibikaji kwa mlaji, ambayo inasisitiza umuhimu wa kumlinda mlaji dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na teknolojia hiyo.”
“Akili nemba inatumika katika shughuli mbalimbali duniani, ni muhimu kwa sababu na sisi ni sehemu ya dunia hivyo suala hilo haliepukiki,” amesema Erio.
Mkurugenzi huyo amesema mlaji ana haki nane na baadhi ya haki hizo ni usalama wa bidhaa na huduma anazopata, haki ya kupata taarifa kuhusu bei, ujazo na malighafi zilizotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali.
FCC ilianza maadhimisho hayo Machi 8, 2024 katika ofisi zake kwa kutoa elimu kupitia redio na mitandao ya kijamii na semina kwa wadau katika sekta mbalimbali.
Mwaka 1980 Umoja wa Mataifa (UN) ulitengeneza kanuni za kumlinda mlaji na kuanzia mwaka 1983 Siku ya Kumlinda Mlaji imekuwa ikiadhimishwa Machi 15 kila mwaka.
Tanzania ilianza kuadhimisha siku hiyo mwaka 2009.