Kanisa Katoliki la Kiaskofu jimbo la Geita lafungwa

Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Flavian Kassala

Muktasari:

  • Kufuatia uvamizi na uharibifu wa mali uliofanywa katika eneo la Altare la Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita Februari 26, Askofu wa Jimbo hilo Flavian Kassala amelifunga kanisa hilo kwa muda.

Geita. Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala amelifunga kwa siku 20 Kanisa Kuu la Kiaskofu la jimbo hilo, kufuatia uvamizi na uharibifu wa mali uliofanywa katika eneo la Altare, baada ya kijana mmoja kuvamia usiku wa kuamkia Februari 26,2023.

Katika taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na Askofu Kassala mwenyewe, imeeleza kanisa hilo limefungwa kuanzia jana Februari 27,2023 na uamuzi huo umetokana na kufuru na unajisi uliofanyika ndani ya Kanisa  hilo.

Amesema uharibifu huo umefanyika kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na unajisi kwa utakatifu wa jengo hilo la kanisa na vifaa mbalimbali vya ibada takatifu.

“Uharifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia Februari 26, 2023 ni kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na umeivunjia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu heshima yake kwa kiasi kikubwa sana na hivyo umeathiri,” amesema.

Amesema uharibifu huo umelinajisi kanisa katika utakatifu wake uliowekwa wakati wa kubarikiwa na uharibifu uliofanywa umeathiri kwa kiasi kikubwa hadhi ya muumini Mkatoliki na jamii kwa ujumla

“Kutokana na matukio hayo, Kanisa hili limepoteza kwa kiasi kikubwa baraka yake na jamii ya waamini imeumizwa sana kutokana na kashfa, kufuru na unajisi uliofanyika kwa imani yetu.

“Hivyo naagiza kwamba Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita halistahili kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi, wala ya Sakramenti yoyote, wala kwa ibada yoyote,” amesema Akofu Kassala.