‘Mafunzo ya kilimo ndio ustawi kwa wakulima wadogo’

Kwa muda mrefu nilitamani kulima kwa tija, lakini sikufanikiwa kufikia malengo yangu baada ya kukosa uelewa na msaada wa haraka kutoka kwa wataalamu wa kilimo. Nililima eneo kubwa lakini nikawa naambulia mazao kiduchu,” anasimulia Lukas Ngole, mkazi wa kijiji cha Image, wilayani Kilolo.

Ngole ni miongoni mwa wakulima waliojitokeza kushuhudia ufunguzi wa kituo cha mafunzo cha Yara, mjini Ilula, mkoani Iringa Machi, 06, 2024.

Licha ya kuwa kilimo ni biashara yenye uwezo wa kuwakwamua wananchi wengi kutoka katika dimbwi la umasikini, wakulima wengi wamekuwa wakilima kwa mazoea, huku wakiambulia hasara kwa kukosa kujua kanuni bora za kilimo na miongozo inayoweza kuwasaidia kulima kwa tija.

Hivyo basi uamuzi wa kufungua kituo hicho karibu na wakulima wa Mkoa wa Iringa unatazamiwa kuwa mkombozi kwa wakulima ambao sasa wana fursa ya kujifunza mbinu nyingi za kilimo na vivutio vingine katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.

Ufunguzi wa kituo hicho utakuwa mwanga mpya kwa wakulima kutoka kilimo cha mazoea mpaka kilimo chenye tija ili kujikwamua na umaskini.

“Nimeua mtaji wangu mara nyingi sana kwa sababu ya mazao duni, katika eka moja ya mahindi nilikuwa naambulia gunia tano tu wakati nimewasikia wenzangu wenye ujuzi wakisema wanavuna mpaka gunia 30 kwenye eka hiyo hiyo moja,” anasema Ngole.

Wapo wakulima ambao tayari wamenufaika na uwepo wa vituo vya mafunzo vya Yara katika maeneo mbalimbali hapa nchini baada ya kupewa elimu na huduma nyingine wezeshi kama vile mikopo ya pembejeo, bima ya mazao na masoko kutoka kwa washirika wa Kampuni hiyo.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes akizungumza baada ya uzinduzi huo anasema ni kweli kwamba kilimo ni biashara ikiwa wakulima watafuata misingi yake.

Anasema Tanzania ina fursa kubwa ya kuleta mapinduzi kwenye kilimo ambacho kinahitaji uwekezaji kutoka kwa wakulima wote wadogo na wakubwa.

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga anasema sasa ni jukumu la wakulima kuchangamkia fursa hiyo inayoweza kuwatoa kwenye umaskini kwa kuwa na uhakika wa kipato cha kutosha kutokana na juhudi za shambani.

“Kazi hii ya kuongeza uelewa kwa wakulima wadogo ambao ndio wazalishaji wengi wa chakula inadhihirisha ubunifu wa sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya Serikali kuimarisha huduma za ugani ili kilimo kichangie katika kukuza uchumi wa nchi na pia kuongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja,” anasema Nyamoga.


Kituo hicho

Kituo hicho kitakachotoa elimu na huduma nyingine muhimu kwa wakulima kutoka wilaya zote za Mkoa wa Iringa, kilifunguliwa kwa ushirikiano wa kampuni ya mbolea ya Yara Tanzania, kampuni ya mbegu ya Seed Co. na Farm For the Future.

Mkurugenzi wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo, anasema ushirikiano wa kampuni hizo ni utekelezaji wa malengo ya kampuni hiyo ya mbolea kuwajengea uwezo wakulima wadogo kwa kuwaletea karibu huduma muhimu, katika uzalishaji wa mazao ya chakula na yale ya biashara.

"Ushirika kuendesha kituo hiki ni uthibitisho kwa vitendo wa dhamira yetu kufanikisha ajenda ya mabadiliko ya kilimo inayochagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuziba pengo la upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kama vile msaada wa mbolea na huduma za ugani kwa wakulima wetu vijijini,” Odhiambo alibainisha.

Anasema watalenga matumizi ya utafiti wa afya ya udongo, kilimo endelevu, kulinda mazingira na kuimarisha mnyororo ya thamani ya kilimo na uzalishaji wa mali shirikishi.

Meneja wa Seed Co. Kanda ya Kusini, Noel Shirima, alisema ushiriki wao ni kutokana na ukweli kwamba, elimu ya wakulima ndio msingi mkubwa wa kutafuta tija katika kilimo na uwekezaji katika eneo hilo litalipa, kwa kuchangia maendeleo endelevu, hususan vijijini ambapo kilimo ndio dawa ya umasikini mkubwa.


Sauti za wakulima

Mkazi wa Kijiji cha Ikuvala, Catherine Sanga, anasema mwaka huu ana uhakika wa kuvuna magunia 30 ya mahindi kutoka kwenye ekari moja baada ya kupata ujuzi na uhakika wa huduma muhimu.

“Miaka miwili iliyopita hali ilikuwa mbaya, mwaka jana nilitumia mbolea ya Yara, nikapata ujuzi kidogo nikavuna gunia 25, lakini mwaka huu mahindi yamestawi sana, nina uhakika wa kufikia gunia 30 hadi 40,” anasema Sanga.

Kwa upande wake, Pasko Ndonde, mkazi wa Kijiji cha Image anasema imani yake kubwa ni kuuaga umaskini kupitia kilimo.

“Binafsi nilikuwa navuna gunia 10 kwa ekari moja, mwaka jana nilivuna gunia 21, lakini mwaka huu, hali ni nzuri. Nimeanza kupikwa kwenye kituo hiki,” anasema Ndonde.

Suzan Muhagama anasema manufaa atakayovuna baada ya kupata elimu ya kilimo kwenye kituo hicho sio tu upande wa kilimo, isipokuwa mpaka kwenye eneo la ufugaji.

“Kazi yetu ni kuja kujifunza tu hapa shambani, binafsi niliposikia kuhusu kufunguliwa kwa kituo hiki sikusubiri nikaribishwe, nilikuja mwenyewe na sasa nina matumaini makubwa. Uelewa umekua,” anasema Suzana.


Mitaji

Mitaji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima wengi kama Susana Wikesi wa mjini Ilula, anayesema pamoja na elimu watakayopata, suala la mitaji linaweza kuwa kikwazo kwa baadhi yao kufikia mafanikio.

“Ardhi imekuwa tatizo, baadhi ya wakulima wanakodi mashamba ili walime, hawamiliki ardhi, sasa kama hawana mitaji sio rahisi kutumia elimu hiyo ipasavyo,” anasema Susan. Hata hivyo, Odhiambo anasema huduma za mikopo ya pembejeo ni kati ya maeneo ambayo vituo vya mafunzo vya Yara hufanyia kazi.

Mwanafunzi anayesomea masuala ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) Egiberty Rubery anasema vijana wengi watapata mwamko wa kuwekeza kwenye kilimo ikiwa watashuhudia namna kinavyoweza kukuza uchumi.