Majaliwa ataja athari za moto Mlima Kilimanjaro
Muktasari:
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezungumzia kuhusu moto uliozuka katika Mlima Kilimanjaro Oktoba 21,2022 ambapo pamoja na mambo mengine amesema umesababisha hasara, hofu na kilometa za mraba 33 za uoto wa asili kuteketea.
Dodoma. Waziri Mkuu Kassim amesema moto uliozuka Oktoba 21, mwaka huu katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaroumesababisha kuteketea kwa kilometa za mraba 33 za uoto wa asili, uharibifu wa mandhari ya ukanda wa juu wa hifadhi na kuteketeza viumbe mbalimbali.
Akizungumza leo Alhamis Novemba 3, 2022 bungeni wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, Majaliwa amesema OKtoba 21, 2022 saa 2.30 usiku iliripotiwa kuzuka kwa moto katika maeneo ya mto Karanga lilopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kinapa.
Amesema Serikali inaendelea kufuatilia chanzo cha moto huo na kuchukua hatua stahiki na jitihada za kuzima moto zimefanyika kwa ushirikiano na wadau mbalimbali hadi kufikia leo Novemba 3 2022.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge wakati wa kikao cha tatu cha mkutano wa tisa wa bunge, jijini Dodoma, Novemba 3, 2022.
“Zoezi la uzimaji moto linaendelea vyema, moto umedhibitiwa kwa kiasi kikibwa katika maeneo korofi. Zoezi la uzimaji linaendelea vyema na moto umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa katika eneo korofi,”amesema.
Amesema shughuli inalendelea vizuri kwa mafanikio makubwa pamoja na changamoto kadhaa ikiwemo upepo wa mara kwa mara unabadilisha mwelekeo.
Ametaja changamoto nyingine ni uwepo wa miinuko mikali makorongo makubwa, mlundikano wa mboji ambayo huifadhi moto kwa muda mrefu na uoto wa mimea ya asili aina ya Erica ambayo inashika moto kwa urahisi na hivyo kusababisha moto kusambaa kwa kasi.
Amesema kuwashukuru wadau wote ambao wamekuwa bega kwa bega kushirikiana na Serikali kuhakikisha moto huo unathibitiwa.
“Ninatoa shukrani za pekee kwa Jeshi la Wananchi Tanzania kutoa helkopta mbili na askari 878 kuongeza nguvu katika uzimaji wa moto ambao umedhibitiwa katika maeneo,”amesema.
Amesema wakati tukio la moto likiendelea katika bonde la Karanga maeneo mengine yaliyobainika kuwa na moto ni maeneo ya hifadhi mlima Kilimanjaro kwenye msitu wa asili wa Ubetu Samanga Wilaya ya Rombo na eneo la Mandara, Marangu.
“Moto ulidhibitiwa na kuzimwa na vikosi vyetu vya ulinzi Tanzania TPDF askari wa jeshi la akiba la hifadhi, mgambo kutoka Wilaya za Rombo na Longido na Jeshi la Polisi kutoka Mkoa wa Kilimanjaro,”amesema.
Amesema tukio hilo limesababisha hasara, hofu na kuteketea kilometa za mraba 33 za uoto wa asili uharibifu wa madhari ya ukanda wa juu wa hifadhi na kuteketeza viumbe mbalimbali.
Amesema hata hivyo kutokana na jitihada za wadau mbalimbali, waliweza kuokoa maeneo muhimu ya utalii ambayo yamebaki salama na hivyo shughuli ya utalii kuendelea kama kawaida.
SOMA ZAIDI: JWTZ kuzima moto Mlima Kilimanjaro
Katika kabiliana na changamoto ya moto inayojitokeza katika maeneo ya hifadhi ikiwemo Kilimanjaro, Majaliwa ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Tanapa na Kinapa kuhakikisha kuwa kinaundwa kitengo ndani ya Tanapa cha kukabiliana na majanga au maafa yanayotokana ndani ya hifadhi.
Pia ameagiza taasisi hizo kuwekeza katika matumizi ya teknolojia ya kisasa husani katika tahadhari utambuzi na uzimaji moto, kuimarisha shughuli za doria na kushirikisha jamii na wadau.