Mifuko ya plastiki yarejea sokoni

Dar es Salaam. Ikiwa imepita takribani miaka mitatu tangu mifuko ya plastiki ipigwe marufuku, kumeibuka aina nyingine ya mifuko ya rangi ya bluu.

Awali mifuko laini isiyokuwa na rangi ndiyo ilikuwa karibu kila sehemu, lakini sasa imekuja aina mpya ya mifuko ambayo tofauti yake inaanzia katika ugumu, ukubwa na hata kuwekewa rangi.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka alipoulizwa na Mwananchi hivi karibuni alisema: “Sijaiona na sijui kama ipo, wakati mwingine hadi tupate taarifa maana wakati mwingine tuko safarini au ofisini.”

Alisema mifuko inayotakiwa kutumiwa sasa ni ile iliyopitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na ikiwa mifuko hiyo haijapitishwa ni kosa kisheria, huku akieleza kuwa hata viwanda vinavyotengeneza mifuko mbadala vinatambuliwa.

Athari za mifuko ya plastiki ni pamoja na kutooza katika mazingira kwa kuwa inakadiriwa kudumu hadi zaidi ya miaka 500, hivyo kuleta athari za muda mrefu, uchafuzi wa mazingira hasa kwa mifuko hii kuzagaa ovyo katika mazingira.

Hata hivyo, uwepo wa mifuko hiyo ya plastiki imetajwa na baadhi ya wafanyabiashara kuwa kama msaada na imeleta ahueni wanapotaka kuwahudumia wateja wao, tofauti na ilivyokuwa bahasha, magazeti na mifuko mbadala. “Mpaka kuwepo sokoni maana yake imeruhusiwa, sisi tumenunua kama kawaida katika maduka ya vifungashio japokuwa tofauti na ile mifuko ya zamani iliyopigwa marufuku ni ndogo zaidi,” alisema Joyna Msalu, mkazi na mfanyabiashara Tabata Relini jijini hapa.

Alisema walau ujio wa mifuko hiyo unasaidia katika ufungashaji wa baadhi ya bidhaa, ikiwamo nyama na samaki wabichi ambao awali ubebaji wake kwa kutumia mifuko mbadala na magazeti ulikuwa mgumu.

“Hii mifuko haina tofauti na ile iliyopigwa marufuku, labda ukubwa, sina uhakika kama hii ukiiweka ardhini inaoza haraka kama ilivyokuwa imekusudiwa,” alisema Luis Jonathan, mkazi wa Tabata.