Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NEMC yampiga ‘stop’ mwekezaji wa chumvi

Muktasari:

  • Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesitisha shughuli za mwekezaji wa uchimbaji chumvi anayefanya shughuli hizo katika kijiji cha Buyuni wilayani Pangani, Tanga jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Pangani. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesitisha shughuli za mwekezaji wa uchimbaji chumvi anayefanya shughuli hizo katika kijiji cha Buyuni wilayani Pangani, Tanga jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

NEMC imefikia uamuzi huo baada ya uwekezaji wake kutishia maisha ya wanyamapori waliopo kwenye hifadhi hiyo na kuwepo kwa uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

Hata hivyo, NEMC limemtaka mwekezaji wa mradi huo kuwathibitishia kama alifanya tathimini ya athari za mazingira kabla ya kuanza mradi huo na kujua ni athari gani zingeweza kujitokeza pindi wanafanya shughuli za uchimbaji wa matuta (vyungu) vya kuvunia chumvi.

Amri hiyo imetolewa jana wilayani Pangani na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Samuel Gwamaka wakati wa ziara ya kukagua eneo hilo, alisema ameufunga mradi huo na endapo mwekezaji huyo atakiuka amri hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa.

Alisema kwa sasa wanasitisha shughuli hizo baada ya kubaini kuwa kimazingira eneo hilo ni nyeti hasa kwa wanyama wakiwemo Tembo wanaotokea hifadhini na kutembea wakati mwingine kukaa kabisa.

Awali, suala la mradi huo liliibuliwa na baadhi ya wadau wa mazingira katika mkutano uliofanyika katikati ya mwaka huu baina yao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo.

Hatua iliyosababisha kuundwa kwa kikosi kazi cha kuuchunguza mradi huo ambacho kilikuja na ripoti iliyoilazimu NEMC kuchukua uamuzi huo kwa mustakabali wa mazingira.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephrahim Mwangomo alisema eneo ambalo mwekezaji huyo anafanyia shughuli zake hutumiwa na tembo kupata chakula.

Alisema mwekezaji huyo alipokwenda ofisini kwao walimshauri asichimbe chumvi bali ajenge hoteli kwa ajili ya watalii lakini, akafanya kinyume jambo ambalo ni hatari.

Mwenyekiti wa kijiji cha Buyuni, Diwani Waziri alisema mradi huo ulianza mwaka 2015 na walimpa mwekezaji huyu ekari 50 aziendeleze.

Alisema kuwa hekari hizo 50 ziliingizwa kwenye mpango wa kufanya maendeleo katika kijiji hicho.

Waziri alisema kuwa mwekezaji huyo amekuwa akiwasaidia katika huduma mbalimbali za jamii ikiwemo kuwachimbia mabwawa ya kupokea maji ya mvua.

“Pamoja na kwamba mwekezaji huyu tulimpatia hekari 50 ili azitumie kwa shughuli zake, tunakiri kwamba hatukuwashirikisha TANAPA wakati wa kufanya maamuzi ya haya ambayo sasa yanaonekana si sahihi,” alisema

Kuhusu wanyama, mwenyekiti huyo alibainisha kuwa wamekuwa wakifika katika eneo hilo la mwekezaji na wamekuwa wakifika hata katika makazi yao wanapoishi.