Nguo alizovaa Lissu alipopigwa risasi kukabidhiwa wazee

Ikungi. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu atapokewa kwa mila za kabila la Kinyaturu kwa nguo zake alizopigwa nazo risasi kutolewa rasmi, kufuliwa na kupewa wazee kwa ajili ya kuzivaa.

Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki tangu mwaka 2010, alivuliwa ubunge Juni 28, 2019 akiwa kwenye matibabu nchini Ubelgiji kwa madai ya kutoonekana bungeni bila Spika kuwa na taarifa ya maandishi na kutojaza fomu ya tamko la mali na madeni.

Mwanasiasa huyo alikumbwa na mkasa wa kupigwa risasi zaidi 30 Septemba 7, 2017 na kujeruhiwa akiwa kwenye gari nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma alipotoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Chadema Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ibrahim Saidi alisema mkutano wa leo utakuwa na ajenda kadhaa, lakini kubwa ni mapokezi ya Lissu kurudi nyumbani.

Alisema Lissu baada ya kupigwa risasi Septemba 7, 2017 alihamishiwa Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi na baadaye Januari 6, 2018 alihamishiwa nchini Ubelgiji kuendelea na matibabu.

Saidi alisema hivi sasa itakuwa mara ya pili kwa Lissu kurudi nyumbani baada ya kufanya hivyo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 akiwa mgombea urais na alipofika Ikungi alifanyiwa mila.

Alisema nguo za Lissu, zikiwamo shati, suruali, koti, viatu na soksi ambavyo vilihifadhiwa vikiwa na damu vitatolewa siku ya Jumatatu (kesho) kwa ajili ya kumwagiwa mafuta aina ya samli na baadaye zitafuliwa na watapewa wazee wazivae hadi zitakapochakaa.

Nguo za Lissu baada ya kupigwa risasi zilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na dereva wa Lissu waliokuwepo katika hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambako Lissu alifikishwa kwa mara ya kwanza baada ya kushambuliwa.

“Mila zitafanywa kwa kuwa Lissu ni mpigania demokrasia, mpambanaji wa kutetea wanyonge, hivyo atavishwa mavazi ya asili ya kishujaa na atapewa supu ya mila ya pole kwa yaliyomsibu kwenye maisha yake,” alisema Saidi.

Saidi alisema supu hiyo itaandaliwa na wanawake watu wazima na itatengenezwa kwa viungo maalumu vya mnyama aliyechinjwa.

“Supu hiyo atapewa na mjomba wake na itawekwa kwenye chombo cha kimila kinaitwa Ukuu. Itatengenezwa kwa utumbo mwembamba, nyama ya kifuani na mapafu, kwa ajili awe mwepesi, kutuliza maumivu ya maisha yake,” alisema Saidi.

Alisema mila hizo ambazo zitafanyika nyumbani kwa familia ya Lissu ni ushirikiano kati ya familia na Chadema.

“Wakati supu inanywewa mmoja wa wajomba zake atakuwa anatamka maneno ya kumpa pole kwa kumuombea apone, awe na amani na awe salama.

“Supu hiyo haitatolewa bure, wazazi wa Lissu watatoa ng’ombe kwa ajili ya kuwapa wajomba zake walioandaa supu,” alisema.


Mkutano wa hadhara

Katika hatua nyingine, Lissu na viongozi wengine wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu John Mnyika, Mchungaji Peter Msigwa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, John Pambalu wa Bavicha watafanya mkutano wa hadhara.

Msafara wa Lissu utaanza mkutano wa hadhara wilayani Manyoni na baadaye utapokelewa Kata ya Mkiwa kwa ajili ya kuja kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika Ikungi Stendi.

Saidi alisema Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe atawasili Ikungi leo akitokea mkoani Arusha.