Tamu na chungu ya kupanda bodaboda usiku

Muktasari:
- Pamoja na faida hiyo ya bodaboda, inapofika usiku usafiri huu unaleta mashaka kwa abiria na dereva anayeendesha chombo hiki. Mashaka haya yanatokana na kila mmoja kukosa imani na mwenzake kutokana na matukio ya wizi na uhalifu ambayo yamekuwa yakihusisha vyombo hivyo yakitokea nyakati za usiku.
Dar es Salaam. Usafiri wa pikipiki ‘bodaboda’ unaotumiwa kwa kiasi kikubwa katika kurahisisha usafiri maeneo ya mijini na vijijini.
Kwenye majiji makubwa bodaboda ni mkombozi dhidi ya foleni ambazo zimekuwa zikisumbua katika barabara nyingi. Kutokana na muundo wake inaweza kupenya na kutembea kwa haraka, kumuwahisha abiria.
Pamoja na faida hiyo ya bodaboda, inapofika usiku usafiri huu unaleta mashaka kwa abiria na dereva anayeendesha chombo hiki. Mashaka haya yanatokana na kila mmoja kukosa imani na mwenzake kutokana na matukio ya wizi na uhalifu ambayo yamekuwa yakihusisha vyombo hivyo yakitokea nyakati za usiku.
Matukio hayo ni pamoja na wizi wa pikipiki, wizi wa fedha na mali za abiria, utekaji na uporaji kwa watembea kwa miguu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Kamishna msaidizi, Janeth Magoni alisema kwa kushirikiana na polisi jamii wamewakamata watu kadhaa wanaojihusisha na mtandao wa wizi wa pikipiki sambamba na pikipiki zilizoibiwa.
“Hali imekuwa shwari sasa baada ya kufanya msako na tunaendelea kuwaelimisha hawa bodaboda kwenye vijiwe vyao wajuane na wajisajili ili akitokea mtu ambaye hawamuelewi watoe taarifa. Pia wasipandishe `mshkaki’ (abiri wawili kwa wakati mmoja) maana ni rahisi hao abiria wakakugeuka.
“Kwa upande wa abiria wasichukue bodaboda hovyo, ni vema kwenda kwenye vijiwe tena kwa wale wanaovaa vikoti, pale madereva wanatambulika na rahisi kuwafuatilia,” alisema Kamanda Magoni.
Mwananchi imezungumza na waendesha bodaboda na abiria ambao wametoa njia saba za kukabiliana na hofu hiyo, ili kuhakikisha pande zote zinakuwa salama. Kwa usalama wa dereva wa bodaboda njia hizo ni kuwa na kijiwe maalumu cha kufanyia kazi na kujisajili kwenye kikundi, kujisajili kwenye `apps’ (kampuni zanazotoa huduma za usafiri) za usafiri mtandaoni, kutofanya kazi usiku wa manane na ikilazimika kufanya hivyo basi afunge mfumo wa ulinzi utakaowezesha kuifuatilia pikipiki ikiibiwa.
Upande wa abiria, njia zilizoshauriwa ni kutumia bodaboda waliosajiliwa kwenye `apps’ (kampuni zanazoendesha usafiri huo) za usafiri, kuchukua bodaboda wanaowafahamu na kuchukua bodaboda anayefahamika kwenye kijiwe husika. Akizungumza na Mwananchi, Athuman Mohamed ambaye ni dereva wa bodaboda, alisema licha ya kuwa usiku ndiyo muda wa kupata fedha kutokana na adha ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam hulazimika kutekeleza majukumu yake kwa tahadhari kubwa.
“Inapofika usiku, binafsi huwa siendi zile sehemu za pembezoni maana kuna wenzangu kama wawili wameshaporwa pikipiki, tena ukiwa na bodaboda mpya ndio hatari zaidi,” alisema Mohamed.
Godfrey Nyanje, dereva wa bodaboda maeneo ya Msongola nje ya jiji la Dar es Salaam naye alisimulia kisa kilichowahi kumkuta dereva mwenzake. “Usiku tunafanya kazi kwa sababu ya shida. Kuna mwenzetu kijiweni alikodiwa na abiria ampeleke Kitonga, kuna sehemu kuna kama pori kumbe yule mtu alikuwa na wenzake wametangulia.
“Alipofika pale porini, yule abiria akadai amebanwa na haja ndogo ajisaidie yule dereva alivyosimama akashangaa amevamiwa, watu wakachukua pikipiki kwa kuwa hakutaka kushindana nao hawakumuumiza sana,”alisema.
Wakati madereva wa bodaboda wakieleza hayo, baadhi ya abiria wameeleza kuwa nao hukosa imani na usafiri huo nyakati za usiku.
Salama Peter, mkazin wa Mbagala alieleza kutokana na mara nyingi kurudi nyumbani usiku mkubwa amelazimika kuwa na mawasiliano ya bodaboda kadhaa anaowafahamu ili kuepuka kuangukia kwenye mikono ya wahalifu.