Tanzania, Italia kushirikiana kuendeleza kilimo

Balozi wa Italia nchini Tanzania, Marco Lombard (katikati) akizungumza jambo wakati wa mkutano wa mafunzo ya kutumia mashine za kilimo za teknolojia za kisasa za nchini Italia. Picha na Pamela Chilongola
Muktasari:
Italia ni miongoni mwa nchi zilizofanya mageuzi makubwa katika kilimo kupitia teknolojia kuanzia upandaji hadi uvunaji
Dar es Salaam. Katika kuunga mkono azma ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza sekta ya kilimo Tanzania, Balozi wa Italia hapa nchini, Marco Lombard amesema nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano maalumu wa wawekezaji wa kilimo kati ya Watanzania na Waitaliano uliofanyika jijini hapa leo Machi 21 2024, Balozi Lombard amesema Italia imefanya mageuzi makubwa katika kilimo kupitia teknolojia kuanzia upandaji hadi uvunaji.
Hivyo, amesema wawekezaji kutoka nchini humo wapo tayari kushirikiana na Watanzania katika eneo la teknolojia ili kilimo kiwe na tija.
Mkutano huo, uliohusisha wadau wa kilimo na kampuni mbalimbali nchini zinazojihusisha na kilimo, umeandaliwa na asasi ya wafanyabiashara kutoka Italia (Italian Trade Agency) kwa kushirikiana na FederUnacoma, ambacho ni chama cha kilimo nchini Italia.
Katika mkutano huo, wawekezaji hao kutoka kampuni zinazojihusisha na kilimo nchini Italia ikiwamo ya Masscar, Barbieri na Ocmis Irrigazione, wameelezea namna bora ya kufanya kilimo chenye tija kwa uchumi wa nchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Mkurugenzi wa FederUnacoma, Fabio Ricci mwaka huu amesema wanatarajia kufanya maonyesho ya kimataifa ya kilimo, kuanzia Novemba 6 hadi Novemba10 mwaka huu.
Amesema maonyesho hayo yatafanyika katika mji wa Bologna, nchini Italia na yameandaliwa na Feder Unacoma.
Amesema zaidi ya mashine 50,000 za aina tofauti zitaonyeshwa, “natarajia mashine hizi zikinunuliwa na Watanzania zitaleta suluhu kwenye shughuli mbalimbali za kilimo ikiwemo kupanda, ulinzi wa mimea na mavuno.”
Aidha, Ricci amesema maonesho hayo yatakuwa ni fursa kwa wadau wa kilimo kutoka Tanzania ambao wataenda Italia kushiriki kwa kuwa watajifunza mambo mengi kuhusu kilimo cha kisasa na fursa zinazopatikana.
“Pia, watajionea zaidi ya mashine 50,000 za kisasa za kilimo zikiwamo za ulinzi wa mimea,” amesema.
Katika mkutano huo, wadau wa kilimo hapa nchini wamefurahia teknolojia za Italia zinazotumika katika kilimo na kutoa wito wa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Mwakilishi wa Tanzania kutoka kampuni inayojishughulisha na masuala ya kilimo ya Italian Trade Agency, Noela Mwamanga amesema wako katika mchakato wa kuchagua kampuni watakazozisafirisha kwenda kushiriki maonesho hayo.
Mwamanga amesema kampuni hizo ni zile zinazojishughulisha na kilimo na safari ya kuelekea Italia itafanyika mwezi ujao.
Amesema Lengo la kuchagua baadhi ya wafanyabiashara wenye kampuni za kilimo ni kutaka kuongeza ushirikiano baina yao na ushiriki wa moja kwa moja kati ya kampuni za Tanzania na Italia.
"Kampuni za mashine za kilimo kutoka Italia ambazo ni Masscar, Barbieri na Ocmis Irrigazione wamekuja kueleza na kutoa elimu kwa wakulima na watumiaji wa teknolojia ya mashine za kilimo nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na wakionesha dhamira ya kampuni za Italia katika kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo,” amesema Mwamanga.
Pia, ameomba msukumo zaidi wa mafunzo kuwekwa kwa wakulima wadogo na wakati, wanaowakilisha kundi kubwa katika sekta ya kilimo ambayo imeajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.