Tindikali ya udongo yatesa wakulima

Muktasari:
- Watafiti wa afya ya udongo wamesema ripoti ya utafiti imebaini maeneo mengi ya nchi yana tatizo la udongo wenye tindikali unaozuia mimea kupata virutubisho, hivyo mavuno kuwa madogo.
Dodoma. Tatizo la upatikanaji wa chokaa kilimo na bei yake limeelezwa kuwaathiri wakulima ambao maeneo yao ya ardhi yana janga la asili la udongo wenye tindikali, inayozuia mimea kama vile mahindi na maharage kupata virutubisho.
Hayo yamebainika leo Jumanne Aprili 9, 2024 kwenye mkutano uliokutanisha wanasayansi, wachumi na wadau wa kilimo wa ndani na nje ya nchi, ikiwamo Ethiopia.
Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) iliyo chini ya Wizara ya Kilimo.
Mratibu wa utafiti wa udongo nchini, Dk Sibaway Mwango katika ripoti ya utafiti wa afya ya udongo, amesema imebainika kuwa maeneo mengi ya nchi yakiwamo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Ruvuma, Katavi, Rukwa na Njombe udongo wake una kiwango cha juu cha tindikali.
Amesema changamoto ya tindikali kwenye udongo inazuia mimea kupata virutubisho, hivyo kutomea vizuri licha ya wakulima kutumia mbolea.
Dk Mwango amesema kutokana na tatizo hilo, walifanya majaribio kwa wakulima wa wilaya za Geita na Mbozi kwa kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa na matumizi ya chokaa kwa ajili ya kupunguza tindikali kwenye udongo, na matokeo yalikuwa mazuri katika uzalishaji wa mahindi na maharage.
“Mfano, wakulima kwenye wilaya hizo, kabla ya matumizi ya chokaa kilimo kwa hekta moja walikuwa hawapati mavuno mazuri, lakini baada ya kuanza kutumia chokaa kuondoa tindikali kwa hekta moja wamevuna hadi zaidi ya tani moja ya mahindi,” amesema.
Dk Mwango amesema katika utafiti wamebaini wakulima wanatumia mbolea nyingi kukabiliana na tindikali wakati wangetumia kilimo chokaa, wangeokoa gharama wanazotumia kununua mbolea.
Ametoa mfano mkoani Ruvuma wamebaini kuna matumizi makubwa ya mbolea, kwa kuwa chache inayowekwa inashindwa kurutubisha mazao kutokana na udongo kuwa na tindikali nyingi.
Dk Mwango amesema katika kukabiliana na hali hiyo, mwezi ujao wataanza kutoa mafunzo kwa maofisa ugavi wa Mkoa wa Geita kuhusu matumizi ya kilimo chokaa.
Kwa upande wake, mratibu wa mradi wa uwekezaji wa usimamizi wa udongo wenye tindikali Afrika (GAIA), Dk Joel Meliyo amesema tindikali kwenye udongo si tishio kwa kuwa inatokana na asili ya ardhi yenyewe, inaweza kusimamiwa katika kuondoa madhara yake kwa kutumia kilimo chokaa au matumizi sahihi ya mbolea.
Amesema tindikali ipo kwenye maeneo mengi ya dunia, lakini kinachofanyika ni kuidhibiti kwa kutumia kilimo chokaa.
Mkulima kutoka Geita, Paschal Lufulila aliyehudhuria mkutano huo, ametoa uzoefu akisema wataalamu kutoka Tari wamemwezesha kulima kilimo cha kisasa na sasa anavuma magunia hadi 20 ya mahindi kwa heka moja, kutoka magunia matano aliyokuwa akipata zamani.
Amesema kilio cha wakulima wa Geita ni upatikanaji wa chokaa kwa kuwa gharama za kuisafirisha kutoka kiwanda kilichopo Dodoma hadi Geita ni kubwa.
“Mwanzo tuliambiwa mfuko mmoja wa kilo 50 za chokaa ni Sh7,000 kwa bei ya kiwandani. Wakulima walichanga fedha wakitaka mifuko 300. Hata hivyo, tulipofika kiwandani tukaambiwa gharama za usafiri ni kubwa. Mfuko mmoja kwa Geita utauzwa Sh11,000,” amesema.
Amesema baadhi ya wakulima walikuwa tayari kununua kwa bei hiyo, ila kinachohitajika ni elimu.