Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upimaji afya udongo kuwanufaisha zaidi ya wakulima 40, 000

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa upimaji wa afya ya udongo na mafunzo kwa wakulima mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Wakulima 40,000 kutoka mikoa ya Mara, Geita, Tabora na Kagera wanatarajiwa kunufaika na mradi wa upimaji wa afya ya udongo na mafunzo kwa wakulima.

Musoma. Wakulima 40,000 kutoka mikoa ya Mara, Geita, Tabora na Kagera wanatarajiwa kunufaika na mradi wa upimaji wa afya ya udongo na mafunzo kwa wakulima.

Mradi huo unaoratibiwa na Kampuni ya kuzalisha mbolea ya OCP Afrika unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh900 milioni ambao pia utaboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo katika mikoa hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo mjini Musoma Juni 30, 2023, Meneja Mradi wa Upimaji Udongo wa OCP,  Kephas Sima amesema watu 10,000 katika vijiji 100 vya mkoani Mara watanufauka na mradi huo.

“Hadi sasa kampuni yetu imekwisha toa mafunzo kwa kwa wakulima 120,000 katika mikoa 12 nchini na lengo letu mbali na kutengeneza na kusambaza mbolea kulingana na mahitaji lakini pia tunataka kuhakikisha afya ya udongo inatambulika na hatimaye kuongeza matumizi bora ya mbolea ili kilimo kiweze kuwa na tija,"amesema

Akitoa taarifa ya hali ya udongo kwa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Idara ya Udongo na Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (Tari), Fredrick Mlowe amesema udongo katika mkoa huo una upungufu wa virutubisho sita vinavyohitajika kwenye upandaji na ukuzaji wa mazao.

“Hapa Mara kuna upungufu wa virtubisho muhimu sita kati ya virutubisho zaidi ya 13 vinavyotajika kwenye mazao na mfano wa virutubisho vinavyokosekana kwenye  udongo wa hapa ni pamoja na salfa, zinc na sulfate kwahiyo matumizi ya mbolea katika kilimo ni jambo la muhimu,"amesema

Meneja Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Kanda ya Ziwa, Dk Asheri Kalala amesema matumizi ya mbolea mkoani humo bado yapo chini hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuhamasisha wakulima kutumia mbolea ili kuleta tija kwenye kilimo.

“Msimu uliopita tulilenga kusajili wakulima 200,000 lakini walisajiliwa wakulima 40,267 tu kwaajili ya mbolea ya ruzuku hiki ni kiashiria kuwa bado tuna kazi ya kufanya kuelimisha  wakulima juu ya matumizi bora ya mbolea,"amesema

Akizindua mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji amesema kilimo cha mazao ya biashara na chakula  mkoani Mara bado hakina tija kutokana na matumizi hafifu ya mbolea.

“Mfano tunavuna tani nne za muhogo kwa hekta moja wakati inatakiwa hekta moja itoe tani 69, mtama tunavuna tani moja kwa hekta badala ya tani tano, sasa hapo mnaweza kuona hali ilivyo,"amesema

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, Mkuu wa wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema mradi huo ni wa muhimu kulingana na uhitaji uliopo.

"Kilimo sasa hivi ni biashara na hatuwezi kulima kwa tija kama tutaendelea kulima kwa mazoea yaani unalima kwa kutegemea ‘Roho Mtakatifu' elimu kwa wakulima ni jambo la muhimu ili waweze kubadilika na kulima kitaalamu," amesema Chikoka