Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Top 3’ ya wagombea urais 2015 hatunao

Muktasari:

  • Kifo cha Lowassa kilichotokea leo Februari 10, 2024 kinakamilisha idadi ya wagombea  watatu vinara wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambao wametangulia mbele ya haki.

Dar es Salaam. Kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa kilichotokea mchana wa leo Februari 10, 2024 bila shaka kimeibua simanzi kwa Taifa kutokana na umashuhuri wake na nafasi alizowahi kuzishika katika maeneo tofauti.

Hata hivyo kifo hicho kinarudisha nyuma watu hadi mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania uliokuwa na upinzani mkubwa, jambo la kusikitisha ni kuwa wagombea wote watatu walioongoza katika uchaguzi huo  wamefariki.

Katika uchaguzi huo wagombea urais walikuwa 8, hayati John Magufuli wa CCM ndiye aliyeshinda uchaguzi huo kwa kura milioni 8.8 hata hivyo kiongozi huyo aliongoza kwa muhula mmoja na miezi kadhaa, kwani licha ya kushinda muhula wa pili alifariki Machi 17, 2021 akiwa madarakani.

Taarifa za kifo cha Rais Magufuli, zilitangazwa na Makamu wa Rais wa wakati huo, Samia Suluhu Hassan (sasa Rais) akisema kiongozi huyo alifariki dunia saa 12 jioni kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa katika Hospitali ya  Mzena jijini Dar es Salaam tangu Machi 6, 2021.

Amesema awali, Rais Magufuli alifikishwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Machi 6, 2021 akisumbuliwa na tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10.

Mshindi wa pili katika uchaguzi huo alikuwa Edward Lowassa aliyegombea kupitia Chadema, alipata kura milioni 6 naye amefariki leo Februari 10, 2024.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango,  Lowassa aliyekuwa na miaka 70, alikuwa akipatiwa matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.

Mshindi wa tatu katika uchaguzi huo alikuwa mgombea wa Chama cha ACT- Wazalendo, Anna Mghwira aliyepata kura 98,763, yeye alifariki Julai 22, 2021 akiwa na umri wa miaka 62.

Mghwira ambaye alikuwa Mwenyekiti wa ACT kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa na hayati Rais John Magufuli mwaka 2017, alifariki katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha alikokuwa akipatiwa matibabu ya changamoto za upumuaji.

Kutokana na vifo vya viongozi hao kwa wanaoamini kuwa kila mwanadamu ana siku yake ya kufa ambayo haibadiliki, bila shaka watakubali kuwa kati ya wagombea watatu waliopata kura nyingi wangeweza kuongoza kwa muhula mmoja tu kikamilifu.

Endapo wangefanikiwa kuchaguliwa kwa muhula wa pili ni wazi kuwa wote wangefia madarakani, hata hivyo kwa wenye imani tofauti kuhusu kifo kwa mwanadamu wao wanaweza kuwa na mtazamo tofauti na huu.


Wagombe walioshika nafasi ya nne hadi nane

Kwa sasa wagombea wa uchaguzi mkuu wa 2015 walioko hai ni aliyeshika nafasi ya nne Chied Yemba wa ADC aliyepata kura 66,049, aliyekamata nafasi ya tano, Hashim Sipunda wa Chauma aliyepata kura 49,256.

Nafasi ya  sita ni Elifatio Lyimo wa TLP aliyepata kura 8,198, wa saba alikuwa ni Kasambala Malik wa NRA aliyepata kura 8,198 na wa nane alikuwa ni Dovutwa Nassoro wa UPDP aliyepata kura 7,785.