TRA Kilimanjaro yasaka wasiotumia mashine za EFD, stempu usiku

Muktasari:
- Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza operesheni ya kukagua matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) na vinywaji visivyo na stempu za kielektroniki (ETS) nyakati za usiku.
Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza operesheni ya kukagua matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) na vinywaji visivyo na stempu za kielektroniki (ETS) nyakati za usiku.
Akizungumza na Mwananchi juzi usiku baada ya ukaguzi katika baa, kumbi za starehe na maduka makubwa, Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Masawa Masatu alisema wanataka kuhakikisha wafanyabiashara wanafuata sheria na mapato ya Serikali yanakusanywa.
“Tumeanza ukaguzi Desemba mosi kwa kuwa Kilimanjaro ni moja ya mikoa inayopata wageni wengi kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na kumekuwa na changamoto ya utoaji wa risiti za kielektroniki, magendo ya vinywaji, uuzaji wa vinywaji visivyo na stempu za kielektroniki na bidhaa bandia.”
Aliongeza: “Wengine tumebaini ni suala la uelewa, wengine ni kutozingatia sheria na wengine elimu wanayo na sheria wanazifahamu lakini hawazifuati, tumechukua hatua kwa wote ambao hawafuati sheria lakini pia wengine tumewapa elimu ili kuweza kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria na taratibu”.
Masatu alisema kuwa sheria inaeleza wazi wale ambao watabainika kufanya biashara bila kutoa risiti za EFD kiwango cha chini cha faini ni Sh3 milioni na kiwango cha juu kikiwa ni Sh4.5 milioni na kwamba wanatakiwa pia kuitafuta kodi iliyokuwa ikipotea ili kuikomboa.
“Kwa wale ambao wanauza vinywaji ambavyo havina stempu za kielektroniki sheria imeweka kiwango cha faini ya Sh5 milioni hadi Sh50 milioni na katika ukaguzi tumeona wapo wafanyabiashara wengi ambao hawazingatii sheria za biashara, bado watu wengi hawatoi risiti za kielektroniki na wanaona suala la utoaji risiti ni la hiari hivyo wana uhuru wa kufanya wanavyojisikia.”
Akizungumza, mmoja wa wafanyabiashara ambao walifanyiwa ukaguzi na maofisa wa TRA, Bruno Ngoo alisema kazi inayofanywa na maofisa wa mamlaka ni nzuri, kwa kuwa inakwenda sambamba na utoaji wa elimu.
“Suala ka utoaji risiti wamiliki wa baa na kumbi hizi za starehe tumekuwa tukielekezwa kila wakati lakini inaonekana hautekelezeki kirahisi, hivyo TRA kuja kufanya ukaguzi usiku huu, kunawafanya hata wafanyakazi wetu kutambua umuhimu wa kutoa risiti kila wanapofanya mauzo.
“Tunajua elimu haina mwisho, hivyo TRA wasiache kutukumbusha kila wakati,” alisema Ngoo.