Vilio vyatawala Lissu akionyesha makovu ya risasi

Muktasari:

  • Mara ya kwanza Lissu kurudi kwao ilikuwa mwaka 2020 alipogombea urais, lakini hakupata nafasi ya kuzungumza na familia yake kuhusu kilichomsibu kwenye shambulio la Septemba 7, 2017 lilitokea jijini Dodoma.

Ikungi. Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ameiliza familia yake baada ya kuwaonyesha makovu ya risasi alizoshambuliwa.

Lissu ambaye amerudi nchini baada ya kuishi uhamishoni kwa takriban miaka saba, jana alifika nyumbani kwako akiwa amerudi rasmi.

Mara ya kwanza Lissu kurudi kwao ilikuwa mwaka 2020 alipogombea urais, lakini hakupata nafasi ya kuzungumza na familia yake kuhusu kilichomsibu kwenye shambulio la Septemba 7, 2017 lilitokea jijini Dodoma.

Baada ya kufika eneo la nyumbani kwao, Mahambe, Ikungi mkoani Singida, Lissi alisimama nje ya uzio wa (nje ya boma) wa makazi yao na wanafamilia wakiwamo shangazi na bibi zake walifanya misa ya kikristo na dua kwa kuwa familia yake ina Waislamu na Wakristo na baadaye walifanya maombi ya kimila.

Shangazi na bibi zake walimwagia maji ya baraka ya kimila kwa lengo la kumtakasa kabla ya kuingia ndani ikiwa na lengo la kuondoa mikosi kutokana na yaliyomkuta.

Mpwa wa Tundu Lissu, Liku Kilindo alisema jana ilikuwa ni siku ya furaha kwa kuwa wanafamilia takriban 100 walikusanyika kwa ajili ya kumpokea mtoto wao.

Alisema licha ya furaha waliokuwa nayo, Lissu aliielezea familia jinsi alivyoshambuliwa, sababu za kuondoka tena mwaka 2020 na sababu za kurejea nyumbani.

Kilindo alisema Lissu alieleza aliondoka tena mwaka 2020 kutokana na kutishiwa usalama wake na alilazimika kwanza kukimbilia ubalozi wa Ujerumani, waliomsaidia kuondoka nchini.

“Familia pia ilielezwa sababu za kurejea nchini kwamba ni kukutana kwake na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Ubelgiji alipomueleza mambo kadhaa ikiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe atolewe jela na kufutiwa kesi, pia maslahi yake ya ubunge.

“Pia, aliwaeleza wanafamilia kuwa sababu nyingine ya kurudi nchini ni kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara,” alisema.

Alisema kwa sasa anajisikia usalama kwa kuwa kufukuzwa nyumbani ni jambo baya.

Shughuli hiyo ilifanyika kwenye boma la baba yake Lissu, Augustine Mughwai Lissu ambaye kwa sasa ni marehemu na eneo hilo lina wanafamilia wengi.

Kilindo alisema shangazi na bibi zake Lissu walimuandalia supu ya kimila iliyoitwa maghili ambayo hupewa mtu aliyetoka kwenye matatizo na hata mzazi pia hupewa supu hiyo.

Alisema pia ameandaliwa chakula cha kimilia kinaitwa daghwa kilichoandaliwa na shangazi na bibi zake kwa ajili ya kumbariki na kuondoa nuksi.

Kuhusu nguo alizokuwa amevaa wakati akipigwa risasi, Kilindo alisema watapewa wajomba zake ambao watazivaa.

Nyamadai, mama mdogo wa Lissu alisema amefurahi kumuona mtoto wao na alicheza ngoma kwa furaha ya kumuona mtoto akiwa hai.

Alisema Lissu aliwaonyesha makovu ya risasi hali iliyowafanya watokwe na machozi na kuwaelezea mkasa ulivyokuwa.

“Tunamuombea Mungu ambariki, makovu haya siyo shida, bora uhai wake. Tumemfanyia vitu vya kimila, tumemwagia maji ya baraka ya kimila na tumecheza miziki ya Kinyaturu,” alisema.

Nyanela, shangazi wa Lissu, alisema wakiwa ndani walitengeneza nguo za mfano wa Lissu na kuzimwagia maji ya baraka, kucheza na kuzivika tasbihi kwa maana Mwenyezi Mungu amlinde na kumbariki.