Wabunge Chadema watoa tathmini ya ushindi ubunge 2020

Dar es Salaam. Wabunge wa Chadema wana imani kuwa iwapo uchaguzi mkuu ujao utafanyika kwa uhuru na haki, watashinda majimbo kutokana na mikakati waliyobuni kukabiliana na hali ya sasa ya kisiasa.

Wabunge hao wamedai utafiti, ambao hawakuwa tayari kuuelezea kwa kina, unaonyesha watashinda uchaguzi iwapo utaendeshwa kwa uhuru na haki.

Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakilalamikia mazingira magumu ya kufanya siasa kutokana na kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara ya kuzungumza na wananchi, kukamatwa mara kwa mara na kuzuiwa kufanya vikao vya ndani.

Lakini John Mnyika, ambaye ni mbunge wa Kibamba, Saed Kubenea (Ubungo) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wamesema tathmini waliyofanya inaonyesha wana uwezo wa kushinda iwapo mazingira ya uchaguzi yatakuwa sawa kwa wote.

Mnyika, ambaye yuko bungeni kwa vipindi viwili sasa, alisema amefanikiwa kuanzisha operesheni aliyodai imemhakikishia nafasi ya kurejea jimboni hapo.

“Tumefanya operesheni ya mtaa kwa mtaa kuandikisha wanachama wapya, kuangalia uhai wa chama na idadi ya wapigakura na tumejihakikishia tuna mtaji wa kutosha,” alisema Mnyika.

Matumaini kama hayo alikuwa nayo Kubenea, ambaye ndio kwanza ameingia bungeni baada ya Jimbo la Ubungo kugawanywa.

Kubenea alisema ripoti ya mwaka huu ya utafiti wa hali ya kisiasa, ambayo hakueleza ilifanywa lini na taasisi gani, imekamilika na ataiwasilisha ofisi za chama.

“Hali nzuri,” alitamba Kubenea.

“Nazunguka jimboni na gari langu, nashiriki misibani, michezo na wananchi wanasema ‘mheshimiwa tunajua mmebanwa kufanya siasa ila bado tuko pamoja na nyinyi’.”

Katika jimbo hilo, Chadema ina mitaa tisa kati ya 46 na kata sita kati ya nane chini ya Ukawa.

Pia Lema, ambaye pia anamalizia kipindi cha pili cha ubunge, alisema CCM haina nafasi ya kupata ushindi ndani ya jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Lema, mmoja wa wabunge waliopata kura nyingi mwaka 2015, Chadema inaongoza kata 16 kati ya 25 na asilimia zaidi ya 51 ya mitaa ndani ya jimbo hilo.

“CCM imeshakufa siku nyingi Arusha. Tutashinda mitaa yote na baada ya hapo tutashinda jimbo katika uchaguzi ujao.”

Arusha ni kati ya maeneo ambayo upinzani uliathiriwa na wanasiasa kujivua madaraka na uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM na hivyo kulazimisha chaguzi ndogo ambazo CCM ilishinda.

Kwa upande wake katibu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM, Kanali Ngemela Lubinga alisema haamini katika utafiti huo wa Chadema kwa kuwa kipaumbele cha Watanzania ni utekelezaji wa ahadi zao, akidai Rais John Magufuli amefanikiwa kutekeleza ahadi za msingi kwa zaidi ya asilimia 100.

“Tunaamini uchaguzi umekuwa wa haki wakati wote,” alisema.

“CCM iliingia Ikulu na ilani yake mwaka 2015 na imetekelezwa hadi kupitiliza kwa hiyo tunaamini Watanzania watatuunga mkono. Kufanya tafiti ni haki yao ila utafiti unaweza kuwa na matokeo hasi na chanya.”