Wanafunzi 9,011 wapata ujauzito kwa mwaka mmoja

Muktasari:

  • Changamoto ya wanafunzi kupata ujauzito na kukatisha masomo imeibuka bungeni ambapo Serikali pamoja na kutaja idadi ya waliopata ujauzito imeelezea utekelezaji mikakati ya kuwawezesha kuendelea na masomo.

Dodoma. Jumla ya wanafunzi 9,011 wa shule za msingi na sekondari walipata ujauzito katika kipindi cha kati mwaka 2021 hadi 2022.

 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameyasema hayo leo Jumanne Januari 31, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Hawa Mchafu.

Katika swali lake la msingi, Mchafu amehoji ni wanafunzi wangapi waliokuwa wajawazito na wangapi wamerejeshwa shuleni baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan wanaojifungua kupata fursa ya kurejea shule.

Akijibu swali hilo, Kipanga amesema katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi wa shule za msingi waliopata ujauzito ni 1,554 na Sekondari ni 7,457.

Amesema hadi kufikia Januari 2023, wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito na kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ni 1,692.

Aidha, Kipanga amesema kwa upande wa elimu ya msingi, Serikali inaendelea kukusanya taarifa za wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito.

Kauli hiyo ilimfanya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuingilia kati kwa kusema takwimu hizo ni kubwa sana kwa shule za sekondari na msingi.

“Tungependa kufahamu kwasababu hawa ni binadamu maana yupo aliyempa huo ujauzito kati ya hawa na wale waliowapa ujauzito ni wangapi ambao wamechukuliwa hatua?” amehoji.

Dk Tulia ametaka kufahamu ni wangapi wamekutwa na hatia mahakamani ili kufahamu sheria iliyopo kama inawalinda watoto hao dhidi ya vitendo hivyo vibaya.

Hata hivyo, Naibu Waziri Kipanga hakupata muda wa kujibu hoja ya Dk Tulia kwani alikwisha kumaliza kujibu.