Wanaodaiwa kusafirisha kilo 51 za heroine, kusomewa maelezo yao kesho

Muktasari:

 Semagoya na wenzake watatu wanatarajia kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vya upande wa mashtaka, kutokana na upelelezi wa kesi yao kukamilika


Dar es Salaam. Serikali imepanga, Aprili 9, 2024  kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka matatu yakiwamo ya kutakatisha Sh62.9milioni na kusafirisha dawa za kulevya aina ya  heroine zenye uzito wa kilo 51.47,  kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao ni Ernest Semagoya, mkazi wa Mbezi Beach, Salim Jongo, Amin Sekibo na Tatu Nassoro.

Washtakiwa hao watasomewa maelezo hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi ameieleza Mahakama hiyo, leo Aprili 8, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo taarifa muhimu zilizowasilishwa Mahakama Kuu, kama zimeshafanyiwa kazi na kukamilika.

Mbilingi amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ajali Milanzi kuwa walikuwa wanasubiri  vijadala vyenye taarifa muhimu kutoka Mahakama Kuu, ndipo waweze kuwasomea maelezo yao, lakini wamepata taarifa kuwa nyaraka hizo zimeshawasilishwa mahakamani hapo.

Hakimu Milanzi amesema vijalada hivyo vimeshawasilishwa mahakamani hapo huku akiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 9, 2024 kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao na mashahidi watakao toa ushahidi katika kesi hiyo.

Washtakiwa wapo rumande kutokana mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa   Septemba 18, 2020 eneo la Temeke Vetenari jijini Dar es Salaam, walikutwa wakiendesha biashara haramu ya dawa kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 51.47, kinyume cha sheria.

Shitaka la pili ni utakatishaji fedha, kati ya Septemba mosi hadi Septemba 8, 2020 katika maeneo tofauti ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, washitakiwa wote, walikutwa na Sh62,970,000, fedha za Msumbiji 7,370 na za Kenya Ksh400.

Pia, walikutwa wakimiliki magari manane ya aina tofauti, kompyuta mpakato moja aina ya Apple, nyumba mbili zilizopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na shamba la eka 19 eneo la Fukayosi Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Ilidaiwa kuwa,  walikutwa wakimiliki mali hizo huku wakijua zilitokana na kosa tangulizi la kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Shtaka la tatu ni kuendesha genge la uhalifu, kati ya Septemba Mosi hadi  Septemba 8, 2020 katika maeneo tofauti ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa wanadaiwa kuendesha genge la uhalifu  kwa kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya.