Waumini waeleza magumu kanisa kufungwa

Jengo la Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Geita. Picha na Maktaba

Geita. Waumini wa Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo Katoliki Geita wamesema tukio la uvamizi na uharibifu wa miundombinu, vifaa na maeneo takatifu, ikiwemo mimbari (altare) linawapitisha katika nyakati ngumu kiimani.

Wakizungumza na Mwananchi jana, baadhi ya waumini walitaja umbali wa kwenda na kurudi katika Kanisa jirani la Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, gharama ya kukodisha bajaji au pikipiki na kukatisha ibada pindi mvua zinaponyesha wanaposali kwenye viwanja vilivyoko nje ya Kanisa Kuu kuwa ni baadhi ya adha na magumu wanayopitia.

Basil Elias, muumini wa kanisa hilo alisema sasa analazimika kutumia gharama ya kukodi pikipiki au bajaji kwenda na kurudi kwenye ibada kanisa jirani la Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, umbali wa zaidi ya takribani kilomita tatu kutoka kanisa lililofungwa.

“Gharama ni kubwa zaidi mtu anapotaka kuhudhuria na kuwahi ibada za asubuhi, hasa kipindi hiki cha mfungo wa Kwaresma,” alisema Basil.

Alisema baadhi ya waumini wanahudhuria ibada zinazofanyika nje kwenye uwanja wa kanisa ambako nako wanakabiliwa na changamoto ya kukatisha ibada pindi mvua inaponyesha.

“Kwa sababu kuna ibada nyingine kwa nyakati tofauti kipindi hiki cha Kwaresma, tumelazimika kutafuta na kufunga mahema,” alisema.

Muumini mwingine, Charles Kigongo alisema wanaolazimika kusali kwenye viwanja vilivyoko nje ya Kanisa Kuu wanakabiliwa na adha ya utofauti wa mazingira na miundombinu ya ibada, ikiwemo eneo la kupigia magoti wakati wa ibada.

“Viti vilivyoko kanisani vinatoa fursa ya kupiga magoti wakati wa ibada bila kuchafuka, tofauti na hali iliyopo kwenye viwanja vya nje na ukumbi unaotumika kwa ibada hivi sasa,” alisema Charles.

Alisema wanaoathirika zaidi ni watumishi wa taasisi za umma na binafsi wanaohudhuria ibada za asubuhi kabla ya kwenda kazini.

Akizungumzia madhara ya kiimani, Charles alisema, “Altare ni eneo takatifu kwetu, ishara ya msalaba na maji ya baraka ni mambo ambayo kwetu hubeba maana kubwa, kitendo cha kugusa na kuharibu vitu hivyo ni kugusa na kuumiza imani yetu.”

Kauli hiyo iliungwa mkono na muumini mwingine, Merysiana Stephen akisema waumini na viongozi wa kanisa hilo wamelazimika kufunga na kuomba toba kwa yaliyotokea na utakaso kwa jengo na eneo lote la kanisa.

Jumapili ya Februari 26, kijana asiyefahamika alivamia na kuharibu vitu mbalimbali kanisani hapo, hali iliyosababisha kufungwa kwa siku 20 kuanzia juzi hadi Machi 18, mwaka huu kutoa fursa kwa waumini na viongozi kufunga na kuomba kwa ajili ya toba na utakaso.

Akituma salamu za pole kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, Rais Samia Suluhu Hassan juzi aliungana na viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii kulaani na kukemea tukio hilo, huku Serikali ikiahidi kushirikiana na Kanisa Katoliki kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa.

Pia Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir ni miongoni mwa viongozi wa dini aliotuma salamu za pole, akisema tukio hilo si tu ni kufuru kiimani, bali pia limesababisha simanzi kwa waumini na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa kijana huyo (jina linahifadhiwa) ni muumini wa kanisa hilo na amewahi kuwa mmoja wa wahudumu kanisani hapo.