Aliyevunja altare kanisani ni muumini, alikuwa amelewa

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala akionyesha moja ya misalaba iliyoharibiwa na mtu ambaye jina lake wala eneo analotoka haijafahamika aliyefanya uvamizi kanisani hapo usiku wa kuamakia Jumapili Februari 26, 2023. Pamoja na kuvunja samani, mtu huyo ambaye tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi pia alivunja Altare na kumwaga Sakramenti iliyoandaliwa kwa ajili ya Ibada. Picha na Maktaba.

Muktasari:

Kijana mwenye umri wa miaka 25 anayedaiwa kuvamia na kuvunja vitu ikiwemo altare la Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Geita amewahi kuwa muumini na mhudumu kanisani hapo na inadaiwa alikuwa amelewa wakati wa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Februari 26, 2023.

Geita. Kijana mwenye umri wa miaka 25 anayedaiwa kuvamia na kuvunjavunja vitu ndani ya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki Geita amebainika kuwa ni muumini na amewahi kuwa mmoja wa wahudumu wa kanisani hapo.

Kijana huyo (jina linahifadhiwa) anadaiwa kuvamia hilo katika tukio lililotokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26, 2023 pia amegundulika kuwa na kiwango kikubwa cha ulevi mwilini wakati wa tukio hilo lililoibua sintofahamu miongoni mwa wakazi wa mji wa Geita.

Pamoja na kuvunja altare, kijana huyo aliyefanikiwa kuingia eneo la kanisa hilo kwa kuvunja kioo cha lango kuu anadaiwa kukivunja Kiti cha Kiaskofu, misalaba na sanamu za kiimani na vyombo vya kuhifadhia ya maji ya baraka ambayo pia aliyamwaga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amewaambia waandishi wa habari leo Jumatatu Februari 27, 2023 uchunguzi wa awali umebaini kuwa alikuwa na kiwango kikubwa cha kilevi mwilini mwake wakati wa tukio hilo lililotokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26, mwaka huu.

“Kijana yule pia amegundulika kuwa siyo tu ni muumini wa kanisa lile, bali pia aliwahi kuwa miongoni mwa wahudumu kanisani kabla ya kuajiriwa kama kibarua katika kiwanda cha pombe,” amesema Kamanda Jongo

Amesema kabla ya kuvamia Kanisani kufanya uharibifu, kijana huyo alionekana akinywa pombe akiwa na wenzake watatu katika moja ya Baa za mjini Geita walikoondoka Saa 7:00 usiku.

Kuhusu swali la namna gani kijana huyo aliweza kuvunja kioo cha lango kuu la kanisa, kuingia ndani na kufanya uharibifu kwenye eneo lenye ulinzi kwa Saa 24, Kamanda Jongo amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mlinzi wa zamu hakuwepo lindoni wakati wa tukio.

“Mlinzi anadai alikuwa eneo lingine la Kanisa kutokana eneo la lindo kuwa kubwa; lakini uchunhuzi unaonyesha kuna uwezekano kuwa hakuwepo kabisa ndiyo maana mtuhumiwa aliweza kuvunja kioo na kuingia kirahisi kanisani bila kugundulika hadi msimamizi wa walinzi alipofika na kubaini kilichotokea,” amesema

Akizungumzia uvamizi na uharibifu uliotokea kanisani, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema tukio hilo limeumiza imani ya viongozi na waumini wa kanisa hilo kwa sababu baadhi ya maeneo yaliyoharibiwa ni matakatifu.

“Licha ya uharibifu wa vifaa na mali vya mamilioni ya fedha; hili tukio ni mbaya kwetu na inahesabiwa kuwa sawa na kufuru kiimani kutokana na maeneo yaliyoharibiwa kuhesabiwa kuwa ni takatifu,” amesema Askofu Kasala akiviomba vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina kubaini kiini cha uvamizi huo.