Zaidi ya Sh1.14 bilioni kutumika maandalizi ya kuupanga Mji wa Kahama kidijitali

Muktasari:
Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga ni miongoni mwa zinazokabiliwa na changamoto ya makazi holela, yanayochangia kuwepo kwa migogoro sugu ya ardhi, maafa ya mafuriko, hali inayoisukuma Serikali kuja na mpango huo uliopo chini ya mradi wa uboreshaji Miji ya Tanzania (Tactic).
Shinyanga. Zaidi ya Sh1.14 bilioni zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya Mpango Kabambe wa Kidijitali (Master Plan) wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Mpango huo unalenga kudhibiti ujenzi na makazi holela ambayo yamekuwa chanzo kikuu cha maafa, ikiwemo mafuriko yanayotokea wakati wa mvua.
Manispaa ya Kahama ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto kubwa ya makazi holela, ambayo yamekuwa chanzo cha migogoro sugu ya ardhi.
Hali hiyo imeilazimu Serikali kuandaa Mpango Kabambe wa Kidijitali kwa ajili ya kupanga na kuboresha mji huo kupitia Mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (Tactic).
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Robert Kwela amesema kuwa Kahama ni moja ya miji inayokua kwa kasi kubwa kutokana na watu wengi kuingia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Amesema ongezeko hilo limekuwa likisababisha miundombinu iliyopo kushindwa kuhimili mahitaji ya wakazi na shughuli zao, hivyo kuongeza presha katika mipango ya maendeleo ya mji.
Kwela ameyasema hayo leo Julai 7, 2025 wakati wa mkutano wa wadau ambao ni wakuu wa idara pamoja na taasisi zinazotoa huduma ndani ya manispaa hiyo, kujadili mpango kabambe wa kidijitali wa upangaji mji wa Kahama.
Amesema kutokana na changamoto ya mipango Miji, kumekuwa na ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi inayotekelezwa chini ya Tactic hususan katika kipengele cha miundombinu ya barabara, kwani maeneo mengine mkandarasi akiwa anaendelea na shughuli zake anakutana na miundombinu ya umeme, mabomba ya maji au waya za kampuni za simu hali inayochelewesha huduma kwa wananchi.
"Tunashuhudia leo tumepitia changamoto kubwa kwenye utekelezaji wa miradi ya Tactic kwenye eneo la miundombinu, kuna mahali ambapo barabara inapita mkandarasi anakutana na nyaya za TTCL, mabomba ya maji, waya za Tanesco, lakini mfumo huu utahakikisha mifumo inasomana kuondoa changamoto hizo," amesema.
Ameongeza kuwa manispaa hiyo ina jumla ya mitaa 32 na vijiji 45, na matarajio ni kuwa baada ya utekelezaji wa mpango huu, maeneo yote yatapangwa rasmi kama mitaa, hivyo kuondoa mfumo wa vijiji.
Mratibu wa Tactic kutoka kampuni ya Urban Solution, Dar es Salaam, Elias Nyabusani amesema lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha mji wa Kahama unakua kwa mpangilio, kwa kuondoa ujenzi na shughuli holela za kibinadamu ambazo zimechangia kuzorotesha hali ya miundombinu na huduma za kijamii.
"Hata sasa ukiangalia namna shughuli zinavyotekelezwa hapa Kahama, hakuna mpangilio unaoeleweka. Barabara zimegeuzwa kuwa maduka, maeneo yanayopaswa kuwa ya mifereji yamejengwa, na mifereji iliyopo imeziba," amesema Nyabusani.
Ameongeza kuwa mpango huo, ambao utatekelezwa kwa mfumo wa kisasa wa kidijitali ushawahi kutumika nchini, utawezesha uchambuzi wa kina wa miundombinu iliyopo, uwezo wake wa kuhudumia watu waliopo, pamoja na huduma zinazohitajika kwa sasa na baadaye.
“Tunalenga kutatua changamoto za makazi, barabara, mifumo ya maji ya mvua, miundombinu ya majitaka, na kuhakikisha kila eneo lina matumizi yake, iwe ni kwa makazi, biashara au viwanda,” amesema.
Maoni ya wananchi
Wakazi wa Kahama nao wamepokea mradi huu kwa matumaini, wakisisitiza umuhimu wa utekelezaji wake kwa haraka ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba kila siku.
"Sisi tunaupokea kwa mikono miwili. Lakini je, utafanikiwa kweli au ni maneno tu? Tunateseka na mafuriko kila mvua inaponyesha kwa sababu hakuna mitaro. Maji hujaa hadi ndani ya nyumba.
“Kama kweli mpango huu utatatua changamoto hizi, basi tutashukuru sana," amesema Maria Ndimbo, mkazi wa Kata ya Majengo.
Naye Juma Mwandu, mkazi wa Kata ya Mhongolo amesema, "barabara zetu hazieleweki. Ikitokea dharura kama moto, hata zimamoto hawajui pa kupita. Hakuna mpangilio wa mji, hivyo hata barabara zilizopo hazitengenezwi kwa sababu hakuna nafasi. Huu mpango unaweza kuwa neema kwetu," amesema.