ACT Wazalendo yaanza mchakato kumpata mrithi wa Zitto

Naibu Katibu Mwenezi wa chama cha ACT Wazalendo, Janeth Rithe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Januari 28, 2024 kuhusu kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichofanyika juzi. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anatarajia kumaliza muda wake Machi 29, 2024  na tayari viongozi kadhaa wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeanza mchakato wa kumpata mrithi wa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe huku wagombea wa nafasi hiyo na nyinginezo watashiriki katika midahalo ya wazi ya kunadi sera zao.

Zitto anatarajia kumaliza muda wake Machi 2024 na mrithi wake atachaguliwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika Machi 5 na 6, mwaka huu baada ya wajumbe kupiga kura.

Mpaka sasa viongozi kadhaa wanatajwa kutaka kurithi nafasi hiyo, baadhi yao ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo – Tanzania Bara, Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti – Zanzibar, Othman Masoud Othman na mjumbe wa kamati kuu, Ismail Jussa.

Wengine ni Katibu Mkuu, Ado Shaibu pamoja na viongozi waandamizi wa chama hicho, Emmanuel Mvula na Issihaka Mchinjita.

Midahalo ya wazi itakayofanyika itatoa fursa kwa wasiokuwa wanachama wa ACT Wazalendo kushiriki, huku wagombea wakinadi sera zao wakieleza mambo watakayokwenda kufanya ikiwapo watashinda nafasi hiyo.

Jana, kikao cha kamati kuu kilifanyika jijini Dar es Salaam na kutoka na maazimio ikiwemo kuanza mchakato wa kumpata mrithi wa Zitto kuanzia Febriari 14, 2024.

Akizungumzia maazimio hayo leo Januari 28, 2028, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma, Janeth Rithe amesema mchakato wa kumpata mrithi wa Zitto utaanza rasmi Feruari 14.

“Uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea utakuwa kati ya Februari 14 hadi 24, 2024 baadaye mkutano mkuu wa chama utafanyika Machi 5 na 6, mwaka huu,” amesema Rithe.

Amesema viongozi watakaopita na kuchaguliwa kuingia kwenye uchaguzi watafanya midahalo ya wazi, ili kutoa fursa kwa umma kuwafahamu.

“Kamati Kuu imeielekeza sekretarieti kuandaa midahalo ya wazi ya wagombea wa chama na ngome za wanawake na vijana, ili kuwapa nafasi wanachama na umma kwa ujumla kuwajua vizuri wagombea kupitia sera zao,” amesema Rithe.

Pia, amesema kwa sababu sera hizo zitanadiwa hadharani, viongozi hao watakapochaguliwa watatangazwa kwa wananchi kupitia mkutano wa hadhara utafanyika Machi 6, 2024.

Kabla ya mkutano mkuu wa chama hicho, utatanguliwa na mikutano ya ngome mbalimbali za chama hicho.

Kwa mujibu wa ratiba yao, mkutano mkuu wa ngome ya vijana utafanyika Februari 29, 2024, mkutano mkuu wa ngome ya wazee unatarajiwa kufanyika Machi Mosi ukifuatiwa na ngome ya wanawake siku inayofuata.

Uteuzi Makatibu

Wakati huohuo, kamati kuu ya chama hicho imefanya uteuzi wa makatibu katika mikoa 27 ya Tanzania Bara na 11 ya Zanzibar.

Walioteuliwa ni Mussa Mbega (Tanga), Yunus Ruhomvya (Kigoma), Bakari Ramadhani (Arusha) Reuben Bujiku (Geita).

Wengine ni Ladislaus Kashonde (Kagera), Stanley Mbembati (Njombe), Vinnie Mtingwa (Morogoro), Sunday Madinda (Dodoma), Karume Mgunda (Mara), Athman Kabogo (Mbeya) na Michael Nyilawila (Songwe).

Vilevile, wameteuliwa Butije Butije (Mwanza), Lilian Mushi (Kilimanjaro), Mtutura Abdallah Mtutura (Selous), Hamis Mahanga (Tabora), Tasilo Milinga (Ruvuma), Paulo Simbachawene (Iringa), Emmanuel Ipini (Singida) na Makalanga Tebe (Simiyu).

Sharifu Hassan Bilal (Mtwara), Omary Gindu (Shinyanga), January Yamsebo (Rukwa), Faustine Khalfan (Lindi), Mwadawa Hamis (Manyara), Bwandu Ndanje (Katavi), Frank Makalanga (Kahama) na Felix Kamugisha (Dar s Salaam).

Hata hivyo, uteuzi wa Katibu wa Mkoa wa Pwani utafanyika wakati mwingine.

Kwa upande wa Zanzibar, Micheweni itaongozwa na Khatib Hamad Shehe, Wete itakuwa chini ya Masoud Juma Mohamed, Chakechake itaongozwa na Saleh Nassor Juma.

Khamis Tahir Awesu Mohamed (Mkoani), Sheha Khamis Ali (Kaskazini 'A'), Abeid Haji Abdallah (Kaskazini 'B'), Othman Moh’d Abdalla (Magharibi 'A'), Salim Ali Khamis (Magharibi 'B'), Mahmoud Ali Mahinda (Mjini), Omar Khamis Haji (Kati) na Kusini ikiwa chini ya Mohamed Kombo Ali.