Babu Duni: ACT inaimarika kwa mikakati ya viongozi

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji akisalimiana na viongozi wa chama hicho baada ya kuwasili kisiwani Pemba. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea na chaguzi zake za ndani kwa ngazi ya mikoa kote nchini na baada ya kukamilisha ngazi hiyo, watakwenda kwenye uchaguzi ngazi ya Taifa ambapo watachagua viongozi mbalimbali ikiwemo nafasi ya Kiongozi wa Chama baada ya Ztto Kabwe kumaliza muda wake.

Pemba. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji amesema kuendelea kuimarika kwa chama hicho maeneo mbalimbali nchini ni matokeo ya mikakati imara iliyowekwa na viongozi.

Duni amesema hayo leo Januari 18, 2024 baada ya kuwasili kisiwani Pemba kwa ziara maalumu ya uchaguzi wa chama Mkoa wa Micheweni.

Amesema wakati chama hicho kiliendelea na chaguzi za mikoa katika maeneo tofauti, Tanzania kumekua na mwitikio mkubwa kwa wanachama kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.

“Uchaguzi huu umetupa viongozi bora zaidi na watendaji. Tunaamini mwaka 2025 utakua wa mageuzi makubwa kwenye uchaguzi mkuu,” amesema

Sambamba na hilo, amesema pia idadi kubwa ya vijana kujitokeza kugombea nafasi kubwa za uongozi ni ishara ya ukuaji wa demokrasia ndani ya chama chao pamoja na kutoa fursa sawa kwa watu wote.

Wakati hayo yakijiri, amewataka viongozi waliopata nafasi ya kuchaguliwa na wasiochaguliwa kuendelea kushikamana na kuwa kitu kimoja.

“Kwenu nyinyi hakuna mshindi wala mshindwa, sote tujenge chama na kuwa kitu moja ili tutimize lengo letu,” amesisitiza.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa chama wamesema ujio wa mwenyekiti wao ni ishara njema ya ushirikiano wa muda mrefu.

Katibu wa mkoa wa kichama wa Chakechake, Saleh Nassor amesema licha ya kuendelea kufanyika kwa chaguzi hizo na kuonekana kuwa zenye upinzani mkubwa, bado wanachama wao wapo imara na hakuna ambaye hajaridhishwa na chaguzi hizo.