ACT yaibuka na hoja kumi madudu ripoti ya CAG

Muktasari:

  • ACT Wazalendo imefanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/21 na kubainisha maeneo kumi yenye kasoro, huku ikiitaka Serikali kuwawajibisha wahusika.

  

Dar es Salaam. ACT Wazalendo imefanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/21 na kubainisha maeneo kumi yenye kasoro, huku ikiitaka Serikali kuwawajibisha wahusika.

Chama hicho kimeeleza kuwa hoja za ukaguzi za CAG kwenye ripoti za ukaguzi za Serikali kuu kuhusu madudu, mashirika ya umma na Serikali za mitaa, zina thamani ya Sh5.8 trilioni ikilinganishwa na Sh3.6 trilioni kwa mwaka 2019/20.

Akiwasilisha uchambuzi wa ripoti hiyo, msemaji wa chama hicho katika sekta ya fedha na uchumi, Emmanuel Mvula alisema CAG imebainisha katika ripoti yake kuwa, mwaka wa fedha 2020/21, jumla ya matumizi yenye thamani ya Sh1.2 trilioni yalifanyika bila kupita mfuko mkuu.

Mvula alisema CAG amebainisha sehemu kubwa ya fedha hizo ilitokana na mikopo na misaada nje ya nchi.

Alisema mwaka 2019/20, Serikali ilitumia Sh2.2 trilioni bila kupita kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

“Matumizi ya fedha za Serikali bila kupita kwenye Mfuko wa Hazina ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi yetu Ibara ya 135(1) ambayo inaelekeza kuwa ni lazima kila fedha ya Serikali itunzwe kwanza kwenye mfuko mkuu kabla ya kutumika na kuidhinishwa na CAG,” alisema Mvula.

Chama hicho kimebainisha madai ya watumishi wa umma jumla ya Sh429 bilioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara yao na stahiki nyingine walizotakiwa kulipwa siku za nyuma kama kanuni zinavyoelekeza.

Mvula alisema ucheleweshaji huo umeshusha morali ya watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao wa kuhudumia wananchi na ndiyo sababu ya kuporomoka kwa utoaji huduma nchini.

Alisema madai ya wazabuni kwa Serikali nayo yamefikia Sh3.6 trilioni, kikiwa ni kiasi kikubwa cha fedha kushikiliwa na Serikali baada ya kupokea huduma kutoka kwa wazabuni bila kuwalipa.

“Hali hii inasababisha mdororo wa uchumi, Serikali inashikilia fedha za makandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma, hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali, wakati mwingine kufukarisha wananchi,” alisema Mvula.

Pia, alisema uvunjaji mikataba kiholela umelisababishia Taifa hasara ya Sh478 bilioni kutokana na mwenendo wa viongozi wa Serikali kusitisha kiholela mikataba ambayo taasisi za Serikali ziliingia na kampuni binafsi ili kutoa huduma.

“Ripoti ya CAG kwenye mashirika ya umma imeonekana kuwa Serikali imebidi kuilipa Kampuni ya Symbion Dola 153.4 milioni za Marekani (Sh352 bilioni), kutokana na kitendo cha kuvunja mkataba wa kufua umeme na kampuni hiyo bila ya kufuata taratibu,” alisema CAG.

“Watanzania wamechoka kubebeshwa mizigo inayotokana na maamuzi holela yanayofanywa na viongozi kwa masilahi yao. Watanzania wamechoka ndege zao kukamatwa ughaibuni na kupata aibu ya kudaiwa kwa sababu tu viongozi wao wamefanya maamuzi kiholela.”

Wizi wa Sh71 bilioni ni miongoni mwa mambo yaliyochambuliwa, akieleza kuwa fedha hizo zimepotea baada ya CAG kubaini miamala imekuwa ikifanyika kwenda Bandari ya Mwanza lakini huko pia hazikupokewa.

“Fedha hizi zilikuwa zikihamishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kati ya mwaka 2015 na 2020. Zilikuwa zinapelekwa kufanya nini hakuna anayejua. Hata CAG hajatoa majibu yanayoridhisha katika eneo hili,” alisema Mvula.

Msemaji huyo wa sekta ya fedha na uchumi, alisema CAG ametoa hoja za ukaguzi kuhusu Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere akisema mradi huo umecheleweshwa kukamilika na kwamba utaligharimu zaidi taifa.

Alisema taarifa ya CAG inaonyesha utekelezaji wa mradi huo katika Bwawa la Nyerere umefikia asilimia 48.02 hadi Desemba 2021, tofauti na matarajio ambayo ilitakiwa kufikiwa asilimia 94.7. Kasoro nyingine zilizobainishwa na ACT ni ubadhirifu wa Sh279.5 bilioni katika miradi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Bandari ya Tanga, mradi wa Mkulazi.

Mvula alisema katika ripoti ya mwaka huu CAG ameeleza kwa kina hali ya mashirika ya umma nchini akisema kati ya mashirika 200 aliyoyakagua, 45 ni ya biashara na yaliyosalia ni ya huduma.

Hata hivyo, Serikali ilitoa ruzuku ya Sh5.9 trilioni kwa mashirika ya umma. Alisema mchwa bado wamejaa kwenye Serikali za mitaa huku halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipata hasara ya Sh10.3 bilioni ambazo hazikuwasilishwa na mawakala na watumishi kwenye halmashauri.

ACT pia wamebaini kuwa mwaka 2020/21 Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulilipa mafao ya pensheni yaliyozidi mapato ya michango kwa Sh767 bilioni.

“Mwenendo huo wa mfuko wa PSSSF, utasababisha kupoteza uwezo wake wa kuwahudumia wastaafu wetu. Tunaitaka Serikali kukamilisha malipo ya deni lake la Sh2.45 trilioni ikiwa sehemu iliyobaki ya deni la michango ya serikali kwa watumishi kabla ya mwaka 1999,” alisema.

Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe alisema sheria ya ukaguzi wa umma inampa mamlaka CAG kupeleka mashauri moja kwa moja kwenye vyombo vya uchunguzi pale anapoona kuna wizi wa moja kwa moja.

“CAG anaweza kuwasiliana na Takukuru, CAG anaweza kuwasiliana na DPP kwa ajili ya kuchukua hatua ambazo zinastahili kuchukuliwa,” alisema Zitto wakati akifafanua kuhusu uwajibikaji kwenye ubadhirifu uliobainika.

Aliongeza kwamba katika kipindi cha miaka 15 ambacho alikuwa mbunge, hakuwahi kuona taarifa ya CAG yenye wizi wa waziwazi kama hii ya mwaka 2020/21, huku akieleza kwamba hayo ndiyo madhara ya kuendesha serikali gizani.