Adaiwa kumuua mpenzi wake kwa madai si mwaminifu

Adaiwa kumuua mpenzi wake kwa madai si mwaminifu

Muktasari:

  • Watu wanne wamefariki  mkoani Geita katika matukio mawili tofauti likiwemo la mwanamke mmoja aliyeuawa na mpenzi wake baada ya familia yake kushindwa kumlipa fedha alizotumia kumtunza kwa ahadi ya kuoana.

Geita. Watu wanne wamefariki  mkoani Geita katika matukio mawili tofauti likiwemo la mwanamke mmoja aliyeuawa na mpenzi wake baada ya familia yake kushindwa kumlipa fedha alizotumia kumtunza kwa ahadi ya kuoana.

Mwanaume huyo anadaiwa kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini mpenzi wake huyo si mwaminifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henrry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa matukio hayo leo Jumatatu Juni 28, 2021 akimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Ester John (28) mkazi wa Ibamba aliyeuawa na mwanaume ambaye hakumtaja jina.

Amebainisha kuwa Juni 13, 2021 mwanamke huyo aliondoka nyumbani akiwa na mtu huyo aliyesemekana kuwa mpenzi wake na baada ya siku kadhaa, mwanaume huyo alianza kuwapigia simu wazazi wa mwanamke huyo akitaka kulipwa fedha alizotumia kumhudumia mwanamke huyo.

Ameeleza kuwa wazazi wa mwanamke huyo walitoa taarifa polisi walioanza uchunguzi na kumkamata mwanaume huyo akiwa na baadhi ya mali za marehemu huku akikiri kumteka  kwamba aliposhindwa kurudisha fedha zake aliamua kumuua na kumzika katika kijiji cha Masota wilayani Bukombe.

Tukio jingine ni  la watu watatu kupoteza maisha na wengine 14 kujeruhiwa baada ya magari mawili waliyokua wamepanda kugongana katika eneo la Chibingo barabara ya Geita –Katoro wilayani Geita.

Amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Christopher Kachwele (70) mkazi wa Geita, Mericiana Kisena mkazi wa Kasamwa na Geofrey Mathias dereva wa Hiace.