Adaiwa kuuawa kwa kuchomwa na kisu kisa Sh5,000
Geita. Mkazi wa Mtaa wa Kivukoni mjini hapa, Lockman Abubakar (21) ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na kijana mwenzake walipokuwa wakidaiana Sh5,000 ambayo ni malipo ya mgawo wa kuchuna ngozi mifugo katika machinjio ya Serikali yaliyopo Mpomvu.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Safia Jongo akizungumzia tukio hilo Agosti 29, 2023, alisema lililotokea Agosti 27, 2023 katika eneo la machinjio wakati vijana hao wakifanya kazi ya kuchuna ngozi mifugo.
“Saa nne asubuhi kwenye machinjio ya Serikali yaliyopo Mpomvu kata ya Mtakuja, mwanamume wa miaka 21 alifariki dunia baada ya kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto na kijana mwenziye mwenye miaka 21 pia, mkazi wa Tambukareli,” alidai Kamanda Jongo.
Alidai kuwa chanzo cha mauaji hayo kilitokana na Abubakar kumdai mwenzake amlipe Sh5,000 zake baada ya kupokea malipo ya kuchuna ngozi mifugo, ndipo ukatokea mgogoro uliosababisha achomwe mara mbili kifuani na mwenzake huyo kwa kutumia kisu alichokuwa akikitumia kuchunia ngozi.
Alisema Abubakar alipoteza maisha muda mfupi alipokuwa akipelekwa hospitali kwa matibabu na polisi wanamshikilia mtuhumiwa kwa taratibu nyingine za kisheria.
Akizungumzia tukio hilo, msemaji wa familia, Alihaji Hamis Mrisho alisema Lockman aliondoka nyumbani alfajiri ya Agosti 27, kwenda kwenye shughuli zake za machinjio, lakini saa tatu asubuhi walipigiwa simu na kuambiwa mtoto wao amechomwa kisu na mwenzake na hali yake ni mbaya.
Alisema wakiwa njiani kwenda machinjioni, walipata taarifa kuwa amepelekwa Hospitali ya mji wa Geita, lakini walipofika wodi ya dharura walimkuta amepoteza maisha.
“Taarifa tuliyosikia walikuwa wanadaiana hela na mtu mmoja ambaye hatumfahamu kwa jina na alipomdai, alimkwida na akamwambia usiponipa hela nitakudunga kisu na kweli akatoa kisu akamdunga na ikawa mwisho wake,” alisimulia mwanafamilia huyo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivukoni, Gidion Alli aliwataka vijana kuepuka hasira zinazosababisha kuchukua sheria mkononi na kusababisha vifo au majeraha.
Jirani wa marehemu, Judith Mathias alisema tukio hilo linashangaza kwa kuwa ni kijana asiye na mgogoro na watu. "Hili tukio la kikatili linapaswa kukemewa na watu wote, pia nawaomba vijana wajifunze kuwa na subira.
Elizabeth Anatory, mkazi wa Kivukoni alisema sababu ya matukio hayo ni mmomonyoko wa maadili na kuwasihi viongozi kila mara kukaa na vijana na kuwaelimisha ili wajitambue.