Afariki kwa kushambuliwa na mamba akizamia samaki

Muktasari:
- Tukio hilo linaelezwa kutokea jana Oktoba 12, 2023 katika hicho, ambapo mmoja wa mashuhuda Anastazia John, amesema kuwa marehemu ameshambuliwa na mamba wakati akifanya shughuli za uvuvi wa kuzamia samaki kwenye mapango ndani ya maji.
Buchosa. Gerald Malonja (58) mkazi wa Nyanguge Mwanza, amepoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba wakati akifanya shughuli za uvuvi katika Kijiji cha Nyamkolechiwa Kata ya Buhuma, Kisiwa cha Kome wilayani Buchosa, Mkoa wa Mwanza.
Tukio hilo linaelezwa kutokea jana Oktoba 12, 2023 mwaka huu katika hicho, ambapo mmoja wa mashuhuda Anastazia John, pia mkazi wa kijiji hicho, amesema kuwa marehemu ameshambuliwa na mamba wakati akifanya shughuli za uvuvi wa kuzamia samaki kwenye mapango ndani ya maji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamkolechiwa, Alex Masinde amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwanaume huyo aliyefariki amefahamika kwa jina la Gerald Malonja.
Mmoja wa wananchi Wilayani Sengerema Omary Athumani anadhani kuwa upungufu wa samaki katika ziwa hilo, huwenda ukawa chanzo cha mnyama huyo kuvizia wa wananchi kisha kuwashambulia ili apate chakula.
Matukio ya mamba kushambulia na kuua watu na wengine kupata ulemavu wa kudumu yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza licha wananchi kupata elimu juu ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Mkoa wa Mwanza wakiongozwa na Ofisa Wanyamapori Daraja la Kwanza, Mohamed Mpita wametuma kikosi kwa ajili ya kukabiliana na mamba katika kijiji hicho, huku akiwatahadharisha wananchi kuwa makini dhidi ya wanyama hao.
Kwa mujibu wa wakazi wa hao kata na vijiji vilivyoko kandokando mwa Ziwa Victoria, wamekuwa katika hatari ya kupoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba na wengine kupata ulemavu wa kudumu wakati wanapofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika ziwa hilo.