Ajali yakatisha uhai wa Padre Kanisa Katoliki Bukombe

Muonekano wa gari ndogo alilokuwa anaendesha Padre Fabian Bundala (Picha ndogo chini) baada ya kupata ajali ya kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Happy Nation.

Muktasari:

Kifo cha Padre Bundala kilitokea muda mfupi baada ya gari ndogo alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Happy Nation.

Bukombe. Ajali iliyohusisha basi la kampuni ya Happy Nation na gari ndogo iliyotokea mjini Ushirombo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imekatisha maisha ya Padiri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikra Maria, Fabian Bundala.

Kifo cha Padre Bundala kilitokea muda mfupi baada ya gari ndogo alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Happy Nation.

Ajali hiyo ilitokea Saa 2:30 usiku wa Julai 6, 2023 katika eneo la Mtaa wa Misheni nje kidogo ya mji wa Ushirombo yaliko Makao Makuu ya Wilaya ya Bukombe.

Mganga mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Bukombe, Dk Nyamhanga Lange amethibitisha kupokelewa hospitalini hapo kwa mwili wa Padre Bundala.

Kwa mujibu wa mmoja wa waumini aliyezungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina, ajali hiyo ilitokea wakati Padre Bundala akienda makao makuu ya Parokia akitokea mjini Ushirombo.

Amesema basi lililohusika katika ajali hiyo ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda mjini Bukoba.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Julai 7, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akiahidi kutoa taarifa zaidi baada ya kupata maelezo ya kutosha kutoka mamlaka husika.

Ingawa jitihada za kumpata Paroko wa Parokia ya Bikra Maria Msaada wa Daima Ushirombo, Padre Peter Kadundu kuzungumzia suala hilo hazijafanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani, taarifa za uhakika zimeithibitishia Mwananchi kuwa Padre Bundala alifikwa mauti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake.

‘’Baada ya ajali ile, Padre Bundala alikimbizwa kwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe ambako nako alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,’’ amesema muumini wa Kanisa Katoliki kwa sharti la kuhifadhiwa jina

Amesema baada ya ajali, Padre Bundala alikibizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kabla ya kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

‘’Wakiwa njiani kwenda Hospitali ya Bugando kupitia mjini Geita, hali ya Padre Bundala ilibadilika ghalfa ikabidi apitishwe kwanza Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita ambako alifariki wakati madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake,’’ amesema muumini huyo