Ajali za ndege majini na mbinu za uokoaji

Muktasari:
Mjadala mkubwa kwa sasa ni kuhusu mbinu za uokoaji wakati ndege ya Precision ilipoanguka kwenye Ziwa Victoria, mita chache kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba juzi.
Dodoma. Moja ya maswali ambayo watu wanajiuliza kwa sasa ni kwa namna gani ilishindikana kuokoa maisha ya watu waliokuwa ndani ya ndege ya Shirika la Precision PW 494 iliyoanguka kwenye Ziwa Victoria jirani na uwanja wa ndege.
Wataalamu wa masuala ya usalama wa anga wanasema watu kwenye ajali ya ndege hunusurika kutokana na mazingira matatu, moja ni uwezekano wa kuokolewa kwa haraka, kwa ajali kutokea jirani na watu au waokoaji kufika kwa haraka.
Jumapili saa mbili asubuhi, ndege ya Precision iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bukoba mkoani Kagera kupitia Mwanza ikiwa na watu 43 ilipata ajali wakati inakaribia kutua mjini Bukoba.
Uwanja wa ndege Bukoba
Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kiwanja cha ndege cha Bukoba kimepakana na Ziwa Victoria, Kaskazini Mashariki mwa mji wa Bukoba umbali wa maili 0.5 kutoka Bukoba Mjini.
Kiwanja hicho kipo katika kundi la daraja la II miongoni mwa viwanja vinne ambavyo vinatoa huduma katika usafiri wa anga (Mwanza, Mtwara, Arusha na Dodoma), pia ni miongoni mwa viwanja ambavyo hupokea ndege na abiria moja kwa moja kutoka na kwenda nchi za nje. Kiwanja kina uwezo wa kuhudumia ndege za ukubwa kama Bombadier Dash 8 -QR 400.
Kiwanja hiki kilianzishwa mwaka 1940 na utawala wa kikoloni baada ya vita kuu ya pili ya Dunia. Baadaye Serikali ya Tanzania ilikikabidhi kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mara baada ya kuanzishwa kwa Mamlaka kwa lengo la kukisimamia, kukiendesha na kukiendeleza.
Kuanzia mwaka 2008, kiwanja hicho kilifanyiwa maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kurefusha njia ya kutua na kuruka ndege kutoka mita 1,200 hadi mita 1,500 kwa kiwango cha lami ili kuwezesha ndege aina ya ATR 42 kutua na kuruka kwa usalama.
Huduma ya Zimamoto na Uokoaji
Kiwanja kina huduma ya Zimamoto na uokoaji katika daraja la 5 kwa mujibu wa miongozo ya ICAO. Huduma hizo zinajumuisha gari moja la kuzima moto na uokoaji aina ya Benz – STK 2800 yenye uwezo wa kubeba maji lita 5,000.
Namna tatu kupona ajali za ndege
Tovuti ya Quora (jukwaa linaloshirikisha watu kukuza maarifa zaidi duniani), lilimnukuu mmoja wa wataalamu wa usafiri wa anga, Adrian Gjertsen akitaja mazingira matatu ambayo yanaweza kuwanusuru watu kutokana na ajali ya ndege.
1- Hali ya hewa watakayokumbana nayo watu waliyomo ndani ya ndege wakati wa ajali (je, wanaweza kuihimili?)
2- Vitu vinavyowazunguka abiria baada ya kupata ajali -kwa mfano ndege kutolipuka na kushika moto.
3- Kama mazingira baada ya ajali ni hatarishi kwa abiria au kuna uwezekano wa kuokolewa kwa haraka, kwa ajali kutokea jirani na watu au waokoaji kufika haraka.
Gjertsen alisema ajali ya ndege kuanguka ardhini au majini, zote mbili hutegemea uwepo wa karibu wa huduma za uokoaji.
Mazingira ya kupona ajali za ndege
Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja kwa sababu inategemea mazingira yaliyochangia ajali yenyewe. Hata hivyo, Bodi ya Taifa ya Usafiri Salama nchini Marekani kufanya uchunguzi wa kitaifa wa ajali za ndege kuanzia mwaka 1983-1999, ilibaini kuwa zaidi ya asilimia 95 ya waliyo kuwa ndani ya ndege zilizopata ajali walinusurika kifo ikiwa ni pamoja na asilimia 55 ya watu waliojeruhiwa vibaya zaidi.
Nafasi ya kunusurika kifo hutegemea kuwepo kwa moto wakati wa ajali, umbali wa ndege angani na sehemu ilipo ndege yenyewe.
Ajali za ndege kwenye maji
Adrian Gjertsen katika maelezo yake alitoa mfano ajali inayoitwa ‘maajabu ya Hudson’. Ajali hii ilitokea New York, Marekani, Januari 2009, baada ya ndege aina ya Airbus A320 ikiwa na abiria 150 kulazimika kutua kwenye Mto Hudson uliopo katikati ya jijini hilo na abiria wote waliokolewa.
‘’Ukipata ajali katikati ya bahari changamoto kubwa itakua jinsi ya kufika salama nchikavu,’’ alisema. Ndege ya Airbus A320 ikiruka kutoka New York hadi Charlotte ililazimika kutua kwa dharura katika mto huo kutokana na matatizo ya injini.
Baada ya ndege hiyo kutua juu ya maji, abiria walipanda kwenye mbawa za ndege na waliondolewa na waokoaji wa boti ambazo zilifika haraka mahali hapo na kuwasafirisha ufukweni.
Kati ya abiria 150 na wafanyakazi watano, hakuna aliyekufa huku wachache walijeruhiwa kidogo. .
Boeing 377 yatua baharini
Oktoba 15, 1956 ndege iliyokuwa ikitoka Honolulu (Marekani) kuelekea San Francisco ikiwa na abiria 24 na wafanyakazi saba, injini mbili kati ya nne zilishindwa kufanya kazi ikiwa angani na rubani aliamua kuishusha kwenye bahari ya Pacific. Hakuna abiria aliyekufa wala kujeruhiwa.