Prime
Nani wa kuwasemea wahadhiri wa vyuo vikuu nchini?

Muktasari:
Yaliyo kwenye makala haya ndiyo hali halisi katika vyuo vikuu vya umma mbalimbali. Muhimu wahusika kuyafanyia kazi.
“Leo niko chuoni kwako, niko ukumbi wa maktaba mpya, naomba nije kukutembelea ofisini kwako”.
Ilikuwa sauti ya rafiki yangu nilipoongea naye kwa simu. Hakuwahi kusoma Tanzania kwa sababu baba yake alikuwa mfanyakazi wa balozi mbalimbali nje ya Tanzania. Hana taswira halisi ya vyuo vya hapa nchini.
Nilinyong’onyea kwa taarifa ya ugeni ule ofisini kwangu. Siyo kwa sababu namchukia ila kwa sababu sikutaka ajue hali ya ofisi yangu.
Huko mtaani amekuwa akikutana nami kama mtu nadhifu na mjuaji sana wa mambo mengi ya siasa za nchi hii.
Niliwaza atakavyonichukulia baada ya kufika ofisini kwangu. Kwa unyonge nilimkaribisha huku nikiwa na hofu kama mwanaume aliyejulishwa kumpa mimba binti wa rafiki yake.
Karibu mgeni wangu
Nikaenda kumpokea na kuongozana naye ofisini. Namkaribisha kiti cha wageni naona anasita kukaa. Nikajua shida iliko.
“Kaa tu kaka, hilo siyo vumbi ndiyo rangi ya kiti. Hicho kiti kimeonja makalio mengi sana tangu alipokuwa anatumia profesa wangu wakati nasoma hadi leo ni hicho hicho”, nilimsihi huku nikiongeza masihara kidogo.
“Daktari, hii ndio ofisi yako? Mbona maofisa wa serikali huko mjini nikienda nawakuta wana ofisi nzuri sana kuliko hii ofisi yako”. Nikajisemea moyoni kuwa huyu jamaa hajaenda Mzumbe, MUST, na SUA akajionea hali za ofisi zao.

Pengine angeanzisha kampeni ya “Punje Punje” kupata pesa za kuboresha mazingira ya kazi ya wahadhiri vyuo vikuu.
Lakini ugeni ule umenitesa sana kwa miezi hii ya hivi karibuni. Nimekuwa nikiwaza sana jinsi wasanii na chawa wanavyotunanga wasomi na umaskini wetu.
Naomba niseme machache ambayo Watanzania hawayajui kuhusu hali ya ufundishaji vyuo vikuu kwa sasa na mazingira yake ya kujifunza.
Ofisi za wahadhiri zinatia huruma
Si ajabu kukuta ofisi inakaliwa na wahadhiri watatu hadi wanne. Wamekuwa kama walimu wa chuo cha Mpuguso au Tandala.
Ofisi zina samani za miaka ya 1980 wakati Nyerere akiwa Rais wa awamu ya kwanza. Viti vya ofisi nyingi vimechoka kiasi kwamba mhadhiri akikalia siku nzima, lazima baada ya mwezi apite MOI kupata matibabu ya mgongo.
Hapo sijaongelea kuhusu meza za ofisi. Unaweza ukadhani labda wahadhiri hawa wameiokosea sana serikali. Maana unaiangalia meza unapata taswira ya meza wanazotumia wauza matunda wa sokoni.
Vifaa vya kazi na nyenzo za ufundishaji
Nimekuta idara kadhaa vyuoni hazina hata wino, karatasi na kalamu. Kuna idara moja walimu wanaenda kwenye ofisi ya mwalimu mwenzao kuchapisha mitihani na mazoezi ya darasani.
Mwalimu huyo asipokuwepo idarani siku hiyo basi hakuna huduma. Mkuu wa idara ana cheo cha jina lakini ofisi yake haitoi huduma kwa wahadhiri.
Siyo hivyo tu, kipindi cha mitihani idara zote zinapeleka mitihani ndakini kwa ajili ya kuchapishwa maana idarani hakuna mashine ya kurudufu mitihani.
Kibaya zaidi wahadhiri wa baadhi ya ndaki walishasahau kama kuna posho za kusimamia mitihani na kusahisha.
Unawaonea huruma wahadhiri ambao wamekuwa kama walimu wa sekondari ya Maposeni ambako huduma nyingine wanafuata shule ya Abasia Peramiho.
Miaka ya 1990 baada ya Serikali kuanza kuelemewa na mzigo wa kugharimia elimu, shule nyingi zilikosa kemikali na vifaa vya maabara.
Serikali ikavumbua mbinu mpya ya kufundisha masomo ya sayansi kwa njia waliyoita ‘alternative to practicals’.
Baadhi ya wanafunzi walipita kwa mfumo huo wakijua kuchora vifaa vya maabara na kuelezea inavyotakiwa kufanya.
Walikuwa na matumaini kuwa ipo siku wakifika chuo watajifunza vizuri. Na kwa kweli walikuwa wanakuta vifaa na kemikali za kutosha kwenye maabara.
Lakini naona ile mbinu ya ‘alternative to practicals’ imeshatufikia na sisi vyuo vikuu. Unaenda idara ya kemia, fizikia,zZoolojia, na sayansi nyingine, hukuti kemikali na vifaa vya maabara, na kama vifaa vipo basi vimejichokea mpaka unawaonea huruma.
Teknolojia ya zamani
Unaenda kule Ndaki ya Uhandisi unamkuta mhadhiri anapambana kuwafundisha wanafunzi wake wa uhandisi wa magari na umeme kwa kutumia teknolojia ya zamani iliyoletwa chuoni miaka ya 1960 kipindi chuo kikiwa tawi la Makerere.
Wahandisi wote waliojenga njia za umeme wa Mtera na Kidato walisomea zana hizo hadi leo enzi za bwawa la Mwalimu Nyerere.
Ukiwasema kidogo kuhusu kupitwa na teknolojia wanakuwa wakali kama mbogo. Lakini ukweli ni kwamba Serikali imevitelekeza vyuo vyetu.
Cha ajabu wakati tunahitaji kuwekeza katika kununua vifaa vipya vya kufundishia, Serikali imeviona vyuo vikuu kama mashirika ya kuzalisha faida. Unashangaa wakuu wetu wanaenda kupelekea gawio serikalini, wakati ndani ya vyuo hali inatia huruma.
Majengo na miundombinu chakavu
Vyuo vikuu kadhaa vimepanua sana kampasi zake. Kuna kilicho na kampasi Lindi, Kagera, Iringa, Mbeya nk. Kingine kinafungua kampasi zake Njombe na sehemu nyingine wanazotamani. Kingine kina kampasi hadi Katavi.
Si uamuzi mbaya, lakini ukitembelea majengo na mazingira ya vyuo hivi vinavyofungua kampasi kama uyoga utajiuliza maswali mengi sana.
Swali kubwa zaidi ni kwa nini vyuo hivi vinakimbilia kufungua kampasi mpya wakati majengo yaliyopo na mazingira yake katika kampasi kuu yanahitaji maboresho makubwa? Ukipita SUA, UDSM, Ardhi, na Muhimbili utaumia kuona majengo na mazingira ya vyuo hivyo yanavyohitaji matengenezo makubwa.
Madarasa yamechoka sana na barabara za ndani ya vyuo zimeharibika vibaya. Vyoo na miundombinu ya majitaka imeharibika mno na ni ya muda mrefu.
Miundombinu hii inahitaji matengenezo makubwa ili kuhimili ongezeko kubwa la wanafunzi vyuoni.
Msongo wa mawazo
Unakutana na mhadhiri ana hasira kuanzia asubuhi hadi jioni. Huwezi kuwalaumu wahadhiri kwa hilo kwa sababu wamekuwa na uraibu wa ‘kusongesha’, kuomba salary advance tarehe 10 ya mwezi, kodi ya nyumba, na mateso ya kubanana kwenye mwendokasi.
Wahadhiri walio wengi wanapoteza kati ya asilimia 40 hadi 70 ya mishahara yao kutokana na makato mbalimbali.
Mhadhiri anakatwa asilimia 25 ya mshahara wake kulipa kodi, na asilimia nyingine za bima yan afya, mfuko wa hifadhi ya jamii na madeni benki.
Ukimsalimia tu anaanza na malalamiko utadhani wewe ndiyo umemsababishia matatizo. Na Ikitokea akajua wewe ni mwanachama wa chama kile, basi hasira zote zitakuwa juu yako.
Matokeo yake wahadhiri wengi wamepoteza kabisa morali ya kazi ya uhadhiri. Huenda wote wanatamani kwenda bungeni kutunga sheria hata kama hawazijui.
Uwezo wa wanafunzi
Wahadhiri wanakutana na shida nyingi zinazohusiana na uwezo mdogo wa wanafunzi, mazingira waliyokulia, changamoto za kifamilia, malezi ya wazazi wa kizazi kipya na nyinginezo.
Kuna changamoto ya uwezo mdogo wa lugha ya kufundishia na kujifunza, yaani Kiingereza. Gazeti la Mwananchi hivi karibuni wametuambia wamekutana na vitimbi vya wanafunzi wa vyuo vikuu hawajui hata mambo madogo tu ya kawaida ambayo anapofika chuoni alitarajiwa ajue.
Mwanafunzi hajui kabisa Kiingereza cha Katibu Mkuu wa Wizara, Mbunge, Jimbo la Uchaguzi! Na wahadhiri wanatakiwa kuwafundisha hadi wajue na wawe Watanzania wenye maarifa na kulifaa Taifa.
Kuna mhadhiri mmoja aliniambia kuna mwanafunzi alitakiwa kufanya jaribio Februari lakini hakufanya. Amemfuata ofisini Aprili akimwambia kuwa hakufanya jaribio.
Alipomuuliza kwa nini hakufanya, akamwambia eti anaishi na dadake huko Chanika na siku ya jaribio hakumwamsha.
Yapo matukio mengi ya aina hii wahadhiri wanakutana nayo vyuoni. Wakati mwingine unakuwa na wakati mgumu kuamua kuhusu tabia hizi za wanafunzi.
Uadui na wanasiasa
Hili la wanasiasa ni ngumu kulisema maana huu ni mwaka wa uchaguzi. Kuna jamaa kaniambia kuwa hata malaika akiingia kwenye siasa lazima atakuwa shetani. Watanzania wanadhani wasomi wa nchi hii hawana msaada.
Ngoja niwaambie kitu kimoja, wanasiasa wa Tanzania wanajua kila kitu, hakuna wasilolijua. Mwanataaluma anaweza kubobea katika eneo fulani na akatoa ushauri kutokana na ubobezi wake, lakini mwanasiasa hatomsikiliza.
Wanasiasa wametufanya wanataaluma tusiwe watu wa kujiamini kabisa. Mazingira ya sasa nchini yametawaliwa zaidi na vitendo vya ukatili vya kundi la Watanzania wenzetu “wanaokasirika kwa niaba ya serikali ”. Hali hii imewafanya wanataaluma wa nchi kuogopa kushauri lolote lile kwa Serikali.
Jamii inataka wahadhiri wawafundishe wanafunzi kuwa wadadisi, lakini wakijua kudadisi masuala yanayoendelea nchini wanaonekana siyo wazalendo.
Wahadhiri nao wamepoteza kabisa uwezo wa kudadisi, nao wanataka kuwa chawa ili ‘watoboe’ kimaisha. Maana wasanii na chawa wanaishi maisha bora na ya uhakika kuliko wahadhiri.
Siku moja pale Mlimani City wakati wa kuzindua sera fulani, wanataaluma tulisimama mstari mmoja. Nyuma yangu alikuwapo mkuu wa taasisi moja ya elimu nchini. Pembeni walikuwa wakuu wengine wa taasisi mbalimbali za elimu. Wale wahudumu wa itifaki wakawaita wasanii waingie kwa njia ya upendeleo.
Msanii alikuwa wa thamani kuliko wasomi wale. Siku hizi wanasiasa wanawaona chawa na wasanii kuwa wa maana zaidi kuliko wanataaluma.
Ombi kwa Chamwino
Tunaomba Serikali irejeshe heshima ya vyuo vikuu hata kama wanasiasa wetu hawawezi kuona umuhimu wa wasomi.
Mazingira ya kufundishia na kujifunza vyuo vikuu yamekuwa yakiporomoka siku hadi siku. Na haishangazi kuona wanataaluma wengi wanajitokeza kugombea ubunge ingawa nako wanakutana na wajumbe wanaowakatilia mbali.
Vyuo vikuu visichukuliwe kama mashirika ya umma ya kuzalisha faida na kujiendesha kibiashara. Bali Serikali ivitazame vyuo vikuu kama taasisi za kuzalisha maarifa na utafiti. Tunahitaji uwekezaji mkubwa kwa kuwaendeleza wahadhiri waendane na mabadiliko ya sayansi ya teknolojia.
Mhadhiri ana maarifa ya miaka ya 1990 aliyopata huko Cambridge enzi hizo na akirudi kazoea kufundisha kwa chaki.
Si ajabu hadi leo nyakati za ufundishaji wa kisasa bado tunaendelea kuagiza chaki za Maswa.
Badala ya kuwa na madarasa ya kisasa, tunaendelea kutumia ubao wa kufundishia kama vile sekondari na shule za msingi.
Nahitimisha kwa kusema mimi ni mjumbe tu, naomba wenye tabia ya visasi na kisirani, waniache huru. Haya niliyosema yafanyiwe kazi, nisifanyiwe kazi mimi mjumbe.
Mwandishi ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (0787525396)