Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tabasamu kwa mabinti wenye ndoto kuwa wanasayansi

Muktasari:

  • Ni mabinti waliokata tamaa ya kutimiza ndoto zao za elimu, lakini sasa Serikali imewaletea tabasamu.

Rozalia Peter kutoka Lindi, alikuwa na ndoto ya kuwa mhandisi wa mitambo tangu akiwa bado mdogo.

Alikuwa mwanafunzi mahiri, akichukua mchepuo wa fizikia, kemia na hisabati katika Shule ya Sekondari ya Lucas Maria Mkonai kwa matarajio ya kujiunga na chuo kikuu.

Lakini ndoto hiyo ilianza kufifia mara tu alipokosa alama za kutosha katika mtihani wa kidato cha sita.

“Maisha nyumbani yalikuwa magumu. Wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunipeleka chuo kingine, na hatimaye niliamua kuolewa. Nilijua elimu yangu imefika mwisho,” anasimulia kwa hisia.

Hata hivyo, simu kutoka kwa rafiki yake ilisababisha mabadiliko makubwa.

“Alinieleza kuwa kuna fursa ya masomo kupitia ‘Foundation Programme’ katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT). Ingawa nilikuwa tayari mjamzito, niliamua kutuma maombi.”

Leo hii, Rozalia amerudi darasani  kupitia ufadhili kamili unaobadilisha maisha ya mamia ya wasichana nchini Tanzania.

Rozalia ni miongoni mwa wasichana zaidi ya 400 waliodahiliwa katika programme hiyo ya msingi chini ya mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (Higher Education for Economic Transformation (HEET).

Mpango huu unasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa msaada wa Benki ya Dunia, na umejikita pia kuwaokoa wasichana waliokosa nafasi ya kujiunga na elimu ya juu kutokana na changamoto za ufaulu, umasikini au ndoa za mapema.

“Huu si mpango wa elimu tu; ni mpango wa kurejesha matumaini na kuwawezesha mabinti,” anasema Sophia Mpokera, Mratibu wa programu hiyo kutoka OUT.

“Ada, malazi, nauli, vifaa vya kujifunzia, bima ya afya, chakula na hata vishikwambi tunatoa  kila kitu kinagharamiwa kwa lengo la kuwaondolea vikwazo vyote.”

Kutoka kukata tamaa hadi azma mpya

Jacklina Furaha, mnufaika mwingine, alimaliza kidato cha sita lakini hakupata nafasi ya chuo kikuu kutokana na kupata daraja la tatu la alama 15. Alijaribu kusoma stashahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) lakini alishindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa ada.

“Nilikata tamaa kabisa. Nikaolewa. Lakini rafiki yangu alinieleza kuhusu mpango huu. Niliomba, mume wangu akanikubalia, na sasa niko shuleni tena nikipambana kufikia alama stahiki. Nimekuja na mwanangu na tunatunzwa vizuri,” anasema kwa bashasha.

Jacklina ana matumaini makubwa ya kurudi UDOM kusomea shahada ya uhandisi wa madini mara baada ya kukamilisha programu hii.

“Mwaka ujao, naamini nitarudi UDOM nikiwa na nguvu zaidi na malengo makubwa.”

Kutoka  Zanzibar, Yusra Ally Yusuph naye ana simulizi kama hiyo. Baada ya kupata daraja la III (alama 15) katika matokeo ya kidato cha sita, alijaribu kusoma stashahada lakini hakuweza kupata mkopo.

“Sikuwa na njia ya kuendelea na elimu. Baadaye nilipata taarifa kuhusu nafasi hii. Maisha yangu yamebadilika. Baba yangu sasa ana matumaini juu yangu kwa sababu naendelea na masomo wala hana uoga tena kwa mimi kutoka Unguja kuja Bara kwa ajili ya elimu,” anasema Yusra.

Njia ya kuziba pengo la kijinsia katika sayansi

Mpango huu umeibuka wakati Tanzania inakabiliana na changamoto kubwa ya uwiano mdogo wa kijinsia katika fani za sayansi na teknolojia. Takwimu kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zinaonyesha kuwa chini ya asilimia 30 ya wanafunzi wa sayansi katika vyuo vikuu ni wanawake.

Mwaka  2022, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilibainisha kuwa ni asilimia 18.4 tu ya wanawake waliokuwa kwenye elimu ya juu walikuwa wakisomea fani za STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati).

“Hili ni jambo la kutia hofu,” anasema Dk Anna Mshana, mtafiti wa elimu ya juu na mtaalamu wa jinsia. Anaongeza:

“Tukishindwa kuwawezesha mabinti kuingia kwenye maeneo haya muhimu, tutakuwa tumeiacha nusu ya jamii nyuma kwenye safari ya maendeleo.”

Dk Mshana anaamini kuwa juhudi za makusudi kama hii ya kupitia mradi wa HEET, ni muhimu ili kufikia ukuaji wa haki kwa wote.

“Hatupaswi kuangalia ufaulu pekee, bali tuangalie pia vikwazo vya kijamii na kiuchumi vinavyowakumba mabinti. Mpango huu ni mfano bora wa namna ya kushughulikia changamoto hizo.”

Programu hii ni sehemu ya mikakati ya Serikali  katika kukuza ushiriki wa wasichana kwenye taaluma za sayansi. Mnamo mwaka 2022, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilizindua Samia Scholarship, mpango unaotoa ufadhili kwa mabinti waliofanya vizuri katika sayansi kwenye mtihani wa kidato cha sita.

Tayari, zaidi ya wasichana 3,000 wamepata msaada wa kusomea shahada katika fani kama uhandisi, sayansi ya afya, na teknolojia ya habari.

Serikali pia imechukua hatua madhubuti kuhakikisha wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba  wanarejea shule. Kufikia mwaka  2024, zaidi ya wanafunzi 18,347 walikuwa tayari wamerudi kwenye mfumo rasmi wa elimu kupitia sera ya kuwarejesha shuleni.

“Hii ni jitihada ya kuandaa kizazi kipya cha wanasayansi wanawake ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya taifa,” anasema Profesa Elifasi Bisanda, Makamu Mkuu wa OUT aliyemaliza muda wake.

Profesa Bisanda anasema kuwa hapo nyuma kulikuwa na wimbi kubwa la wanafunzi hasa wa kike ambao kwa kukosa tu alama fulani, walishindwa kutimiza ndoto zao na kuachana na shule, jambo ambalo kwa sasa ni tofauti.

“Hawa wasichana, asilimia kubwa nimewashuhudia wakifaulu na kujiunga na vyuo vikuu. Hatuna shaka na programu hii, maana imesaidia kuokoa kizazi chenye uwezo mkubwa lakini kilikuwa kinatupwa nje ya mfumo kutokana na matokeo,” anaeleza.

Programu hiyo ya msingi imeundwa mahsusi kuwaandaa wanafunzi kwa elimu ya sayansi ya kiwango cha chuo kikuu. Wanaohitimu hupata sifa ya kujiunga na shahada katika vyuo vya umma na binafsi nchini.

Wanafunzi pia hupata sifa ya kupata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na ile ya Zanzibar (ZHESLB).

“Tayari baadhi ya wanafunzi kutoka kundi la kwanza wanaendelea na shahada zao katika vyuo kama UDSM, SUZA, UDOM na vingine.Katika kipindi cha miaka mitano ya mradi, tunatarajia kuona ongezeko kubwa la wanawake kwenye taaluma za sayansi,”anasema Mpokera.

Ufadhili huu umeondoa karibu kila kikwazo cha kifedha. …“Tunawapa nauli za kwenda na kurudi, vishikwambi vyenye bando kwa ajili ya kujifunzia kidijitali, chakula kamili, bima ya afya na mazingira rafiki kwa wazazi kwani wengine wamekuja na watoto wao na wasaidizi,” anafafanua.

Kujenga kizazi kipya cha wabunifu

Kwa kuzingatia ongezeko la mahitaji ya wataalamu wa STEM duniani, mpango huu unalenga kuwajengea mabinti wa Kitanzania uwezo wa kuwa kizazi kinachofuata cha wanasayansi, wahandisi na wabunifu.

“Sayansi si maabara tu au mlinganyo. Sayansi ni namna tunavyoweza kutatua changamoto kama mabadiliko ya tabianchi au usalama wa chakula,” anasema Dk Irene Malecela, mshauri wa sera za ubunifu.

Anaongeza: “Tusipowekeza kwa kizazi cha sasa katika elimu ya sayansi, tutaikosa nafasi ya kuwa na mshindi wa kwanza wa Nobel wa sayansi kutoka Tanzania.”

Kwa kina Rozalia, Jacklina, Yusra, na wengine wengi, programu hii si tu elimu, ni uzima wa ndoto walizozika.

“Hii ni safari ya matumaini, uthubutu na uthabiti,” anasema Jacklina… “Nataka mwanangu huyu anapokua aone kwamba hata ukikwama, bado unaweza kuinuka tena. Hiki ndicho kinachoendelea katika maisha yetu sasa.”

Kwa Taifa, hadithi hizi binafsi zinaunganishwa kuwa simulizi ya taifa linaloendelea kuwekeza kwenye ndoto za mabinti wake. Taifa ambalo halimuachi nyuma msichana yeyote mwenye ndoto ya kuwa mwanasayansi.