Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi awapa neno vijana matumizi ya lugha za kigeni  

Muktasari:

  • Awataka kuacha kutumia lugha za kigeni katika mazingira yasiyostahili, badala yake waitumie lugha ya Kiswahili kwani ndio msingi wa umoja, amani na mshikamano.

Unguja. Kutokana na utandawazi kuchukua nafasi kubwa katika maisha, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein  Mwinyi amewataka vijana na jamii kuacha kutumia lugha za kigeni katika mazingira yasiyostahili, badala yake waitumie lugha ya Kiswahili kwani ndio msingi wa umoja, amani na mshikamano.

Hayo ameyasema leo Julai 7, 2025 katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika maadhimisho ya Siaku ya Kiswahili  Duniani (Masikidu) yaliyofanyika kitaifa, Zanzibar.

"Tusiache kujifunza lugha na utamaduni wa watu wengine lakini tuitumie Lugha ya Kiswahili,  kwani ni rasmi na inatumika katika vyombo vya kimataifa hivyo tusitumie lugha za kigeni sehemu ambazo hazistahili," amesema Dk Mwinyi. 

Dk Mwinyi amesema, lugha hiyo imepata hadhi kwa kuendelea kukua na mataifa mengine kuona umuhimu wa kuitumia katika maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kidiplomasia nchini.

Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwahimiza wadau na viongozi kuhamasisha matumizi lugha ya lugha hiyo kupitia mabaraza yao.

"Ni wajibu wetu sote kuitumia lugha ya Kiswahili na kuifundisha kwa ufasaha wake kwani hatua hiyo itasaidia kuieneza lugha ya hiyo ulimwenguni na katika hadhi yake," amesema Dk Mwinyi 

Mwandishi wa vitabu vya Kiswahili Tanzania, Nyambari Nyangwine amesema kauli hiyo inapaswa kuungwa mkono kwani kufanya hivyo ni kuenzi na kulinda utamaduni.

 Amesema Kiswahili ndio maono ya kisiasa, hivyo ni wajibu wa viongozi wote kuitumia katika majukwaa yao ya kisiasa.

Kwa upande wake,  Mhadhiri wa Kiswahili wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, Dk Ahmad Sovu amesema kauli ya Dk Mwinyi imekuja katika wakati mwafaka.

Amesema vijana ndio nguzo ya Taifa na ndio watumiaji vizuri wa mitandao na hilo litachochea ubora na usanifu wa lugha.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema wanaitumia siku hiyo katika kuienzi kwani ndio alama na utambulisho wa Afrika na urithi wa vizazi.

Amesema kuwa, sherehe hiyo kufanyika Zanzibar haikuwa kwa ajali bali imestahili kutokana na  visiwa vya Zanzibar kuwa mstari wa mbele kuikuza lugha hiyo kwa kuisanifisha na kuipeleka duniani.

Pia, alitoa wito kwa Baraza la Kiswahili Zanzibar  (Bakiza) kutengeneza kamusi za lahaja mbalimbali kwani itakuwa hazina kwa kuzihifadhi ili zisaidie katoa misamiati mipya inapohitajika.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Dk Saade Said Mbarouk amesema Serikali zote mbili zinafanya juhudi kubwa za kukipeleka Kiswahili duniani,  hivyo licha ya viongozi kuonesha jitihada hizo mabaraza na wadau wa Kiswahili wanapaswa kuungana nao katika kutekeleza wajibu huo.

Akitoa salamu kwa niaba ya  Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Nancy Mwaisaka amesema  Kiswahili ni lugha ya mshikamano kwani ndio lugha ya kwanza kutambuliwa duniani na kutumika katika kukuza mshikamano wa watu.

"Tuna kila sababu ya kuifanya lugha Kiswahili inastawi na kuwa chombo kikuu cha kuendeleza amani nchini," amesema.