Wizara ya Elimu yazindua mwongozo wa utoaji mikopo na ufadhili

Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein akizindua muongozo wa utoaji mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Muktasari:
- Wanafunzi wametakiwa kusoma kwa makini mwongozo wa utoaji mikopo kupitia tovuti rasmi ya wizara kabla ya kuwasilisha maombi yao
Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imezindua mwongozo mpya wa mikopo na ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), sambamba na kufungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa waombaji wapya mwaka wa masomo 2025/2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo Julai 6, 2025 Naibu Waziri wa wizara hiyo, Ali Abdulgulam Hussein amesema dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia leo hadi Agosti 31.
Pia, Gulam ametoa wito kwa wanafunzi wote kusoma kwa makini mwongozo wa utoaji mikopo kupitia tovuti rasmi ya wizara kabla ya kuwasilisha maombi yao.
"Serikali imetenga Sh35 bilioni kwa mwaka huu wa masomo kutoka Sh25 bilioni mwaka wa fedha 2024/25, ili kugharamia mikopo na ufadhili kwa wanafunzi 14,618, kati yao wanafunzi wapya 4,877 na wanaoendelea na masomo ni 9,741 katika vyuo vya ndani na nje ya nchi," amesema Abdulgulam.
Wizara hiyo imepongeza juhudi za Serikali kwa kuendeleza uwekezaji katika elimu na kuhakikisha vijana wanapata fursa ya kujiendeleza kitaaluma.
Pia, amesema kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB) itaendelea na utaratibu wa kuanzisha vituo vya msaada wa maombi ya mikopo kwa waombaji wapya katika Kituo cha Sayansi na Ubunifu Jang’ombe kilichopo Unguja ambapo kwa upande wa Pemba kituo kitakuwa Maktaba Kuu ya Chake Chake.
Ameeleza kuwa, majina ya wanafunzi watakaopata mikopo yatatangazwa Oktoba 2025 kupitia akaunti walizotumia wakati wa kuomba, pia amesisitiza mikopo ya vyuo vya nje itatolewa kwa fani ambazo hazipatikani nchini na zenye ushindani ikiwamo udaktari, huku ngazi ya diploma ikiondolewa kwenye orodha ya wanufaika kwa vyuo vya nje.
Wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake Mei 26 katika Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa, ameeleza kuwa ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi unasababishwa na Serikali kuchelewa kupeleka fedha katika bodi ya mikopo.
Amewataka wawakilishi kuhamasisha urejeshaji wa mikopo ili kuongeza ufanisi.
Pia, Waziri Lela amesema Serikali inapanga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na ufadhili wa SMZ kutoka 75 mwaka 2024/25 hadi 85 mwaka 2025/26.