AKU yaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti
Muktasari:
- Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa Juni 5 kila mwaka ambapo taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinaitumia siku hiyo kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) nchini Tanzania kimeshirikiana na wanafunzi wa shule za msingi za Muhimbili na Olympio kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na maua.
Kwa kuwa kaulimbiu ya kimataifa ya maadhimisho hayo ni “Pinga uchafuzi wa plastiki”, walitumia fursa hiyo pia kuongeza uelewa juu ya changamoto za plastiki kimataifa na pia kubuni mbinu endelevu zaidi za kudhibiti hali hiyo.
Wakati plastiki zikiwa na faida nyingi kwa maisha ya sasa, taka za plastiki ni shida inayotambulika ndani ya nchi na kimataifa. Plastiki zinachukua mamia ya miaka kuharibika, inachukua nafasi muhimu katika maeneo ya kutupa taka na inachafua mazingira na bahari.
Mwanafunzi wa AKU, Khadija Ismail Suleiman aliyeshiriki katika hafla hiyo amesema mazingira na hali ya hewa ni kipaumbele cha kimkakati na mada mtambuka chuoni hapo.
“Katika kuongeza thamani ya AKU zaidi, chuo kikuu kiliamua kuadhimisha Siku ya Mazingira kwa kuhamasisha juu ya usimamizi wa taka hasa plastiki miongoni mwa wanafunzi ambao ni mawakala wakuu wa mabadiliko ya utamaduni wa uendelevu na uvumbuzi,” amesema Khadija.
Amebainisha kwamba uchafuzi wa plastiki unazidi kuwa janga duniani, kwa hivyo AKU inalenga kutoa maarifa na ujuzi muhimu miongoni mwa wanafunzi juu ya usimamizi na utenganishaji sahihi wa taka hizo.
Kutokana na hali hiyo, chuo na wafanyakazi walipanda miti 40, maua 20 na kuzipatia shule hizo mapipa ya kuhifadhia taka ili kuwezesha uhifadhi mzuri wa taka.
Amesema AKU kama mtetezi wa mabadiliko ulimwenguni, inafikiria kubadilisha matumizi ya plastiki kwa kugeukia zile zinazotumika mara moja, wanapandikiza maarifa kwa wanafunzi juu ya kuchakata chupa za plastiki kwa matumizi mengine kama vile kupanda maua ili kupendezesha mazingira yao.
“Tunaamini kwamba wanafunzi watakuwa mabalozi wazuri nyumbani kwao na kwingineko katika kueneza zaidi ujuzi wa kusimamia matumizi ya plastiki,” amebainisha.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Muhimbili, Aika Mgeni amesema tukio hilo liliendana na maadili ya shule ya kuweka mazingira safi na nadhifu
“Kama unavyoweza kushuhudia, mazingira ya shule yetu ni safi na yamepambwa kwa miti na maua. Tunashukuru AKU kwa kuunga mkono juhudi zetu,” alisema Mgeni akionyesha kwamba kupitia klabu ya mazingira ambayo imeanzishwa na AKU, wanafunzi wao watakuwa mabalozi wazuri wa usimamizi wa mazingira.
Mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Muhimbili, Haroun Juma ameahidi kutumia vyema ujuzi wa kutumia chupa za maji za plastiki kupanda maua na kutunza vitalu vidogo vya mboga nyumbani na kwa kuwafundisha wenzake.