Aliyebaka mtoto na kumwambukiza ukimwi afungwa maisha mara mbili

Selemani Gwabuga akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha. Picha na Mary Sanyiwa.
Muktasari:
- Selemani Gwabuga amehukumiwa kifungo cha maisha mara mbili na kutakiwa kulipa fidia ya Sh30 milioni na faini ya Sh5 milioni pmaoja na adhabu ya kiboko 11 baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ya kumbaka mtoto na kumwambukiza virusi vya Ukimwi.
Iringa. Mkazi wa Kitongoji cha Idodi, Isimani mkoani Iringa, Selemani Gwabuga (78) amehukumiwa kifungo cha maisha mara mbili na kutakiwa kulipa fidia ya Sh30 milioni na faini ya Sh5 milioni pamoja na adhabu ya viboko 11 baada ya kukutwa na makosa matatu
Selemani ameshtakiwa kwa makosa ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka (11) aliyekuwa anasoma darasa la tano, kuambukiza Ukimwi kwa makusudi na kujaribu kubaka.
Akisoma hukumu hiyo Hakim Mkazi Mkuu, Said Ally Mkasiwa amesema mtuhumiwa amekutwa na hatia ya kubaka bila kuacha shaka kwamba alimbaka mtoto wa miaka 11 na kumwambukiza Ukimwi kwa makusudi huku akijua kuwa yeye ni mwathirika na anatumia dawa za ARVs.
Aidha ilielezwa mahakamani hapo kuwa Selemani ambaye ni maarufu kwa jina la Msabato alikuwa akiishi katika kitongoji hicho jirani na familia ya mtoto huyo ambapo mara kadhaa alikuwa akihubiri injili.
Katika vielelezo vilivyopelekwa mahakamani hapo vilionyesha kuwa Mtuhumiwa Seleman aligundulika kuwa na virusi vya Ukimwi tangu mwaka 2016 katika Kituo cha Afya Mahuninga na kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo.
Inadaiwa kuwa Gwabuga baada ya mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo baada ya kumaliza, alimpa mtoto huyo Sh200 huku akimsisitiza asiseme kwa mtu yeyote.
Lakini katika tukio jingine mtuhumiwa huyo alikutana na mtoto huyo mtoni na alipojaribu kumkazimisha mama wa mtoto huyo alitokea kisha mzee Gwabuga alikimbia lakini tayari alikuwa ameonekana ndipo taratibu za kumkamata zilifanyika.
Hata hivyo, mwaka 2019 alihamia eneo la Idodi na aliendelea kutumia dawa hizo za ARVs huku mama wa mtoto alipimwa na kukutwa hana maambukizi.
Kwa upande wake mtuhumiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu afya yake siyo nzuri na umri wake ni mkubwa miaka 78.
Awali, akizungumza mbele ya mahakamani hiyo kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Burton Mayage aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa sababu ugonjwa aliomuambukiza mtoto huyo hauna tiba na atadumu nao katika kipindi chote cha maisha yake ya mtoto huyo lakini pia amemwathiri kisaikolojia.
Kesi hiyo ilisimamiwa na waendesha mashtaka wawili wa Serikali Nashon Saimon pamoja na Baton na ilikuwa na mashahidi wanne akiwemo daktari aliyempima mtoto huyo na kuthibitisha kuwa alikuwa ameingiliwa na kusababisha kuambikizwa virusi vya Ukimwi.
Katika hatua nyingine faini pamoja na fidia waendesha mashtaka watalazimika kufungua kesi ili mali za mtuhumiwa huyo ziweze kuuzwa na fedha yake kumfidia mwathirika ambaye ni mtoto huyo.