Aliyechomwa moto na mamaye ashindwa kufanya mitihani la saba
Maofisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu walipomjulia hali mtoto wa miaka 13 aliyemwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto na mama yake mzazi wakati walipokwenda kumtembelea katika hospitali ya KCMC alikolazwa.
Muktasari:
- Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalumu imelaani vikali tukio la mwanamke mmoja wa kijiji cha Reli juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, kummwagia mwanaye wa kiume wa miaka 13 mafuta ya taa na kisha kumtia moto kwa madai ya kupika chips na kula wakati alipohisi njaa.
Moshi. Serikali imelaani tukio la Ikiwa mtoto wa miaka 13, mwanafunzi wa kumwagiwa mafuta ya taa na kisha kuchomwa moto na mama yake mzazi kwa madai ya kupika chips na kula wakati aliposikia njaa.
Kutokana na tyukio hilo, mtoto huyo (jina linahifadhiwa) aliyekuwa akisoma darasa la saba katika shule ya msingi Reli Juu, Wilaya ya Mwanga, ameshindwa kufanya mitihani yake ya kumaliza shule iliyofanyika Septemba 14 na 15 mwaka huu baada ya kulazwa Hospitali ya KCMC Moshi akiuguza majeraha aliyopata.
Tukio la kuunguzwa mwanafunzi huyo lililoripotiwa na Mwananchi Digital, lilitokea Agosti 31, 2023 baada ya mama yake mzazi kudaiwa kumfunga mikono na miguu kwenye mti na kisha kumwagia mafuta ya taa na kumtia kiberiti na kisha kutoweka kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumtembelea mtoto huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum, Baraka Makona amesema kitendo hicho hakivumiliki na hakikubaliki.
"Tumekuja hapa kutokana na tukio lililotokea wilayani Mwanga, ambapo Agosti 31 mwaka huu mtoto wa miaka 13 alichomwa moto na mama yake mzazi
“Inasemekana mtoto alikuwa na njaa katika kujitafutia chakula alichukua viazi kwa ajili ya kujitengenezea chipsi, lakini kwa kitendo hicho ambacho nyuma ya pazia tulikuwa hatujui kwa nini kilimkasirisha mama na kununua mafuta ya taa akamwagia mtoto wake na kumchoma moto," amesema.
Amesema mtoto huyo ameungua takribani asilimia 70 ya mwili wake wote na una majeraha makubwa.
“Tunalikemea hili tatizo kwasababu kama mama mzazi ambaye tunamtegemea ndiye mlinzi namba moja wa mtoto mahali popote pale alipo anamchoma mtoto wake, ni jambo la kushangaza na linatia sana fedheha nchi yetu," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema mtoto huyo walimpokea akiwa na majeraha ya kuungua moto na kwamba kutokana na hali yake ilivyokuwa aliingizwa ICU ambapo kwa sasa anaendelea vizuri na yupo wodini.
"Kwa sasa ameshatoka ICU, yupo wodi ya kawaida anaendelea kupata huduma, hospitali imejitoa kuhakikisha huyu mtoto anapata huduma stahiki. Niwahakikishie Watanzania kwamba huyu mtoto anapata huduma na hakuna changamoto yoyote," amesema Profesa Masenga.
Naye Mwenyekiti wa moafisa ustawi wa jamii nchini, Martin Chuwa amewaagiza maofista katika wilaya hiyo, kufanya uchunguzi wa kijamii katika eneo ambalo tukio hilo lilitokea kuangalia kama kuna shida yoyote ya kijamii iliyopelekea mama huyo kufanya kitendo hicho.
"Mtu yoyote anaweza kufanya tukio kama hili hata mzazi anaweza kufanya tukio kama hili kama atapata tatizo la akili, sisi kama maofisa ustawi wa jamii tunatafsiri hili kama kuna shida kwenye akili ya yule mama, japo sio rahisi mtu kuelewa hilo japo mtu anatembea mzima kabisa lakini ukichunguza vizuri sio mzima," amesema.
"Tumeshauri akipataikana huko alipo wakati polisi wakiendelea na kesi zao za kijinai tunaomba afikishwe hapa hospitali ya KCMC na wenyewe hii taarifa wanayo waje wapite kwenye vipimo waangalie kama ana afya njema ya akili,” amesema.
Awali alipotafutwa baba mzazi wa mtoto huyo, Jamadu Msemo amesema taarifa alizozipta kutoka kwa majirani ni kwamba, mke wake huyo aliamua kufanya kitendo hicho kwa madai kuwa mwanaye huyo alimchukulia Sh20,000.