Prime
Aliyeponzwa na lifti, akatupwa jela miaka 20 aachiwa huru

Jinsi alivyojitetea kortini
Katika utetezi mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Haika alikiri kuwa katika gari lililokuwa likiendeshwa na Anthony Chibarangu na kwamba alipewa tu lifti kutoka Kimara anakoishi kwenda Manzese kumtembelea rafiki yake wa kiume.
Njiani gari hilo lilisimamishwa na maofisa wa Jeshi la Polisi ambao waliwaweka chini ya ulinzi. Alikana kusaini hati ya kukamata mali eneo la tukio bali alitakiwa kuisaini Mikocheni katika ofisi za kikosi kazi cha kupambana na ujangili.
Pia alikanusha kutoa maelezo ya onyo ya kukiri kosa mbele ya shahidi wa tatu wa upande wa mashitaka na kwamba, hakuwahi kuulizwa swali lolote linalohusu kutenda kosa linalomkabili na maelezo yaliandikwa nje ya muda.
Mahakama iliridhika kuwa ingawa shahidi pekee ambaye ni wa kwanza wa upande wa mashitaka ndiye aliyetoa ushahidi kwamba alikutwa na meno hayo, iliona ushahidi wake ni bora kuliko hata kuwa na mashahidi wengi, hivyo kuamua kumtia hatiani.
Hakimu alimhukumu kifungo cha miaka 20 kwa kila kosa na kwa makosa matatu, alihukumiwa kwenda jela miaka 20 kwa kuwa vifungo vyote vingetumikiwa kwa pamoja.
Alikata rufaa Mahakama Kuu lakini ikatupwa.
Majaji walivyochambua
Katika kesi ya rufaa iliyowasilishwa Mahakama ya Rufaa, majaji watatu walisema maelezo ya onyo ya mshitakiwa yaliwahi kutolewa katika kesi ya uhujumu uchumi namba 36 ya 2015 dhidi ya Haika, lakini Mahakama iliyakataa.
“Tunavyoona jaji hakuifanyia kazi vizuri hoja ya maelezo hayo, bali alirahisisha mambo. Kama hakimu mkazi mmoja katika mahakama hiyohiyo alisema hayastahili kupokewa kama kielelezo alitakiwa naye alione hilo ilipoletwa mara ya pili,” inaeleza sehemu ya hukumu.
“Tunaona kuwa uamuzi wa mahakama hizo mbili (Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi) kuhusu kupokea maelezo hayo kama kielelezo haikuwa sahihi, kwa hiyo tunaifuta kwenye mwenendo wa kesi hii,” inaeleza hukumu.
Kuhusu ushahidi wa shahidi wa kwanza ambao mahakama za chini ziliona unaaminika na ndio ambao ulimtia hatiani pia, jopo la majaji walijiuliza ilikuwaje hadithi ya shahidi huyo pekee iliaminika lakini ya mrufani (Haika) haikuaminika.
“Swali la pili ni kwa nini Abel Joram, ofisa wanyamapori aliyeshiriki sana hadi kuandaa mtego siku ya tukio hakutoa ushahidi kwenye kesi. Swali lingine ni kwa nini Anthony Philemon ambaye ni mtuhumiwa wa pili hakushitakiwa pamoja na Haika,” walihoji majaji katika hukumu hiyo.
“Kwa maoni yetu, Mahakama Kuu ilifanya kosa kwa kutofanyia upya uchambuzi wa ushahidi kwa sababu ni wajibu wa mahakama kama chombo cha kwanza cha rufaa kufanya hivyo. Hii inatufanya tuvae viatu vyao na kuona hoja tatu za rufaa zina mashiko,” nasema hukumu hiyo.
“Tunatilia shaka uaminifu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza kwa sababu hakueleza kwa vipi Anthony Philemon anayeonekana hadi kwenye cheti cha ukamataji mali alipotelea hewani. Kuacha kumshitaki mshirika wake kunaleta shaka,” inaeleza hukumu.
Majaji katika hukumu wanaeleza, “Kama shahidi huyo wa kwanza angekuwa mwaminifu angeiambia mahakama nini kilitokea kwa Anthony Philemon (ambaye walikamatwa pamoja na Haika) ambacho kiliwazuia polisi au chombo kingine cha dola kumshitaki.”
Majaji walisema kwa kuwa maelezo ya kukiri kosa yameshaondolewa kwenye mwenendo wa shauri hilo, uaminifu wa ushahidi wa shahidi huyo wa kwanza unapoteza nguvu, hasa kwa kuwa upande wa mashitaka uliacha kuita mashahidi wengine muhimu.